Na STELLA ARON, JamhuriMedia, DAR ES SALAAM

Uwekezaji katika teknolojia, kuimarika kwa mifumo ya ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu, utaalamu wa watabiri na ushirikiano wa kimataifa ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuchangia kuongezeka kwa usahihi wa utabiri wa hali ya hewa nchini Tanzania, pamoja na kuifanya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutambulika zaidi kwa wananchi na wadau.

Katika miaka ya hivi karibuni, huduma za utabiri wa hali ya hewa nchini Tanzania zimeendelea kupata nafasi kubwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii. Kuanzia wakulima wanaotegemea mvua, wavuvi wanaokwenda baharini, sekta ya usafiri hadi mamlaka zinazoshughulikia majanga, taarifa za hali ya hewa zimekuwa sehemu muhimu ya kufanya maamuzi.

Takwimu za TMA zinaonesha kuwa utabiri wa mvua za Oktoba hadi Desemba 2023 ulikuwa na usahihi wa asilimia 91.9, huku utabiri wa Novemba 2023 hadi Aprili 2024 ukiwa na usahihi wa asilimia 84.2. Aidha, TMA iliripoti usahihi wa asilimia 94.1 katika utabiri wa msimu wa Vuli wa mwaka 2025/2026.

Mafanikio hayo yanaashiria kuimarika kwa uwezo wa mamlaka katika kukusanya taarifa, kuchambua mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa tahadhari zinazoweza kutumika katika kupanga shughuli mbalimbali.

Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa kiwango cha usahihi hutegemea aina ya utabiri, kipindi kinachotabiriwa na namna matokeo yanavyopimwa. Usahihi wa utabiri wa msimu hauimaanishi kwamba kila utabiri wa kila siku au kila eneo unafikia kiwango hicho.

UWEKEZAJI KATIKA TEKNOLOJIA ZA KISASA

Moja ya sababu zinazochangia kuongezeka kwa uwezo wa TMA ni uwekezaji katika vifaa na mifumo ya kisasa ya kufuatilia na kutabiri hali ya hewa.

Serikali imewezesha ununuzi na ufungaji wa vifaa 10 vya hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga (AVIMET), vituo 50 vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe (AWS), vipima mvua 60 vya kisasa na vituo 15 vya hali ya hewa-kilimo.

Vifaa hivyo vina mchango mkubwa katika kukusanya taarifa za mvua, joto, unyevunyevu, upepo na mabadiliko mengine ya anga kwa wakati.

Tofauti na mifumo inayotegemea zaidi vipimo vya mikono, vituo vinavyojiendesha hurahisisha ukusanyaji na usambazaji wa taarifa kwa wakati, hivyo kupunguza ucheleweshaji na kusaidia watabiri kupata takwimu zinazohitajika katika kufanya uchambuzi.

Pia, mifumo ya rada za hali ya hewa imeongeza uwezo wa kufuatilia mifumo ya mvua na dhoruba inapoendelea kujitokeza. Kwa mujibu wa taarifa za TMA, rada zilizofungwa Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma na Mbeya zimeimarisha ufuatiliaji wa mifumo ya hali ya hewa katika maeneo mbalimbali nchini.

Teknolojia hizo zinapounganishwa na takwimu za vituo vingine, huongeza wigo wa taarifa zinazoweza kutumiwa kutengeneza utabiri.

KOMPYUTA YENYE UWEZO MKUBWA WA KUCHAKATA TAARIFA

Sababu nyingine ni kuimarishwa kwa uwezo wa kuchakata na kuchambua taarifa nyingi za hali ya hewa kwa kutumia kompyuta zenye uwezo mkubwa.

TMA imewekewa kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuchakata taarifa (High Performance Computer – HPC), pamoja na mfumo wa kisasa wa utabiri wa hali ya hewa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a katika maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani, Machi 23, 2026, uwekezaji huo umeimarisha uchakataji na uchambuzi wa data na kuboresha uandaaji wa utabiri na taarifa mahsusi kwa watumiaji wa sekta mbalimbali.

Umuhimu wa teknolojia hii ni kwamba utabiri wa hali ya hewa unahitaji kuchanganua taarifa nyingi zinazohusiana, zikiwemo joto la bahari, mwelekeo wa upepo, unyevunyevu na mifumo ya shinikizo la hewa.

Kompyuta yenye uwezo mkubwa huwezesha matumizi ya modeli za kihisabati na kimazingira kuchakata taarifa hizo kwa haraka zaidi, kuonesha hali zinazoweza kujitokeza na kusaidia wataalamu kufanya maamuzi kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi.

Kadiri taarifa zinavyoongezeka na mifumo ya uchambuzi inavyoboreshwa, ndivyo uwezekano wa kutengeneza utabiri unaoendana na hali halisi unavyoweza kuimarika.

KUIMARIKA KWA VITUO VYA UANGAZI NA UKUSANYAJI DATA

Utabiri sahihi hauanzi kwenye kompyuta pekee, bali huanzia kwenye upatikanaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa kutoka maeneo mbalimbali.

Anasema kuwa TMA imeendelea kuimarisha mifumo ya uangazi wa hali ya hewa ili kupata taarifa za kuaminika zinazotumika kufuatilia mabadiliko ya anga na kutengeneza utabiri.

Kupitia mpango wa Systematic Observations Financing Facility (SOFF), Tanzania inashirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Taasisi ya Hali ya Hewa ya Denmark (DMI) kuimarisha vituo vya uangazi, mafunzo ya wataalamu na mifumo ya kubadilishana taarifa.

Lengo la mpango huo ni kuiwezesha Tanzania kuzingatia viwango vya Mtandao wa Kimataifa wa Uangazi wa Hali ya Hewa (GBON) ifikapo mwisho wa mwaka 2026.

Jitihada hizo ni muhimu kwa sababu hali ya hewa haina mipaka ya nchi. Mabadiliko yanayotokea katika Bahari ya Hindi au maeneo ya nchi jirani yanaweza kuathiri hali ya hewa nchini Tanzania.

Kwa hiyo, kadiri taarifa za uangazi zinavyokuwa nyingi, sahihi na zinazopatikana kwa wakati, ndivyo wataalamu wanavyopata msingi mpana wa kutengeneza utabiri.

UTAALAMU WA MAFUNZO YA WATABIRI

Teknolojia peke yake haiwezi kutoa utabiri unaotegemewa bila kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kuitumia.

Watabiri wa hali ya hewa wanahitaji kuelewa sayansi ya anga, mifumo ya mvua, mabadiliko ya tabianchi na namna ya kutafsiri matokeo ya modeli mbalimbali za utabiri.

TMA imeendelea kuimarisha uwezo wa watumishi wake kupitia mafunzo ya kitaalamu, ikiwemo mafunzo yanayofanyika nje ya nchi, ili kuongeza ujuzi wa kutumia vifaa na mifumo ya kisasa.

Uwezo wa wataalamu kulinganisha matokeo ya modeli na hali halisi, kutambua mabadiliko yasiyo ya kawaida na kufanya marekebisho ya kitaalamu una mchango mkubwa katika kuboresha ubora wa taarifa zinazotolewa.

Hili pia linaonesha kuwa mafanikio ya utabiri yanatokana na ushirikiano kati ya teknolojia na maarifa ya binadamu.

USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KATIKA KUBADILISHANA TAARIFA

Hali ya hewa ya Tanzania huathiriwa na mifumo mikubwa ya anga na bahari inayovuka mipaka ya nchi.

Kwa sababu hiyo, ushirikiano na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), taasisi za kikanda na mamlaka za hali ya hewa za nchi nyingine ni muhimu katika kupata taarifa zinazosaidia uchambuzi.

Kupitia mifumo ya kimataifa ya kubadilishana data, taarifa za uangazi kutoka maeneo mbalimbali duniani zinaweza kutumika katika modeli za utabiri.

Mpango wa SOFF unaotekelezwa Tanzania kwa kushirikiana na UNDP na DMI unalenga pia kuimarisha ukusanyaji, uchakataji na ushirikishanaji wa data kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Ushirikiano huo unaongeza uwezo wa wataalamu wa Tanzania kufuatilia mifumo ya hali ya hewa inayoweza kuathiri nchi, badala ya kutegemea taarifa za ndani pekee.

KUBORESHA NAMNA TAARIFA ZINAVYOWAFIKIA WANANCHI

Kuongezeka kwa utambuzi wa TMA hakutokani na usahihi wa utabiri pekee, bali pia namna taarifa zinavyotolewa na kutumiwa na wananchi.

Katika kipindi cha nyuma, baadhi ya watumiaji walilalamikia ugumu wa lugha iliyotumika katika taarifa za hali ya hewa. TMA imeendelea kuboresha uwasilishaji wa taarifa ili ziwe rahisi kueleweka na kutumika katika shughuli za kila siku.

Kwa mujibu wa TMA hutumia tovuti, mitandao ya kijamii, mikutano ya wadau na njia nyingine za mawasiliano kusambaza utabiri na kupokea maoni ya watumiaji.

Mabadiliko hayo yana umuhimu mkubwa kwa sababu taarifa sahihi isiyomfikia mtumiaji kwa wakati au isiyoeleweka inaweza kushindwa kumsaidia kufanya maamuzi.

Kwa mfano, mkulima anahitaji kujua kipindi kinachotarajiwa kuwa na mvua ili kupanga shughuli za kilimo, wakati mvuvi anahitaji taarifa za upepo na mawimbi ili kufanya maamuzi kuhusu usalama wa safari yake.

Kadiri wananchi wanavyopata taarifa zinazoeleweka na zenye manufaa katika maisha yao, ndivyo wanavyopata nafasi ya kutambua umuhimu wa huduma za TMA.

MATUMIZI YA MREJESHI WA WANANCHI, WADAU

Mrejesho kutoka kwa watumiaji wa utabiri ni nyenzo muhimu katika kuboresha huduma. TMA imekuwa ikikutana na wadau wa sekta mbalimbali kujadili utabiri wa misimu iliyopita, changamoto zilizojitokeza na namna taarifa zilivyosaidia kupanga shughuli zao.

Maoni hayo husaidia kubaini maeneo ambayo taarifa hazikueleweka vizuri, changamoto za utoaji wa huduma na mahitaji ya sekta mbalimbali.

Kwa mujibu wa TMA, mrejesho wa wakulima, wavuvi na wadau wengine umechangia kuboresha namna taarifa zinavyowasilishwa na kuongezeka kwa uelewa na imani ya watumiaji.

Hata hivyo, mrejesho wa wananchi kuhusu manufaa ya utabiri ni tofauti na kipimo rasmi cha kisayansi cha usahihi. Vipimo vya kitaalamu vinahitaji kulinganisha utabiri na hali halisi iliyotokea kwa kutumia vigezo vinavyofanana.

UMUHIMU WA TMA NCHINI

Kadiri utabiri unavyotumika katika maamuzi ya kila siku, ndivyo umuhimu wa TMA unavyoonekana zaidi katika jamii.

Katika sekta ya kilimo, taarifa za mvua husaidia wakulima kupanga muda wa kupanda na matumizi ya pembejeo. Katika sekta ya usafiri, taarifa za hali mbaya ya hewa husaidia kupanga safari na kuchukua tahadhari. Kwa wavuvi, taarifa za upepo na mawimbi husaidia kupunguza hatari za safari za baharini.

Septemba 11, 2026, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, aliipongeza TMA kwa kutoa utabiri wenye usahihi wa zaidi ya asilimia 80, akieleza mchango wake katika kusaidia Serikali na wananchi kuchukua tahadhari mapema dhidi ya majanga ya asili.
Habari

Hali hiyo inaonesha namna utabiri wa hali ya hewa unavyohusishwa moja kwa moja na usalama wa maisha, ulinzi wa mali na mipango ya maendeleo.

MAFANIKIO YANAYOPASWA KUENDELEZWA

Kwa ujumla, kuongezeka kwa usahihi wa utabiri wa hali ya hewa na kutambulika zaidi kwa TMA kunahusishwa na mchanganyiko wa uwekezaji wa Serikali katika teknolojia, kuimarika kwa vituo vya uangazi, uwezo wa kuchakata data, utaalamu wa watabiri, ushirikiano wa kimataifa na kuboresha mawasiliano kwa wananchi.

Hata hivyo, mafanikio hayo hayamaanishi kuwa changamoto zote zimeondoka. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa Aprili 2025 ilibaini mapungufu katika uchakataji na uhakiki wa data, pamoja na changamoto za usajili na usimamizi wa vituo vya hali ya hewa.

Hivyo, hatua inayofuata ni kuendeleza uwekezaji huo, kuhakikisha vituo vinafanya kazi kwa ufanisi, kuimarisha uhakiki wa utabiri na kuhakikisha tahadhari zinawafikia wananchi wote wanaozihitaji.

Mafanikio ya TMA hayatapimwa kwa asilimia ya usahihi pekee, bali pia kwa kiwango ambacho taarifa zake zinasaidia kuokoa maisha, kulinda mali na kuwezesha wananchi kufanya maamuzi yenye tija.