Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

VYOMBO vya habari vinaisaidia serikali katika kuona na kuchukua hatua, hivyo uwepo wa sheria zinazotekelezeka kunaweza kusaidia tasnia hiyo kuwa msaada mkubwa kwa serikali.

Kauli hiyo ilitolewa na Salome Kitomari, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN) katika Kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa na Televisheni ya ITV.

“Tunaona umuhimu wa kufanya mabadiliko katika sheria hii kwa sababu, habari ni maendeleo lakini habari inaisaidia Serikali kufanya maamuzi, inaisaidia Serikali kuona mambo ambayo wakati mwingine inaweza isiyaone.

“Kupitia kalamu ya mwandishi,yanaibuliwa mambo ambayo yanaisaidia serikali kufanya maamuzi na kuchukua hatua mbalimbali.Kwa hiyo,habari ni kwa ajili ya maendeleo,”alisema Salome ambaye pia ni Mhariri wa Gazeti la Nipashe.

Wadau wa habari nchini wanapigania mabadiliko ya sheria ya habari kwa kuwa habari ni sehemu muhimu katika maendeleo ya Taifa.

Amesema,Sheria ya Habari ya Mwaka 2016,imeunda vyombo vingi vinavyosimamia kazi moja ya tasnia ya habari na kwamba,hakuna sababu ya kufanya hivyo.

“Kuna Bodi ya Ithibati, kuna Mfuko wa Waandishi pia kuna Baraza Huru la Vyombo vya Habari. Hakuna sababu yakuwa na vyombo vyote hivi.

“Tena Waziri amepewa mamlaka ya kuteua wajumbe,kwa mfano Bodi ya Idhibati watateuliwa na waziri,sasa uhuru wa hii Bodi ya Ithibati upo wapi ikiwa waziri ndio mwenye mamlaka ya kuteua hawa watu?” amehoji Salome.

Pia amesema,sehemu ya mapendekezo ya mabadiliko ya sheria za habari, imeelekeza kwamba kosa la kitaaluma litatuliwe kitaaluma na si vinginevyo.

“Sisi kama wanataaluma, tunapendekeza kosa la kiaaluma litatuliwe kitaaluma, sheria imeishatutambua kama wanataaluma basi hata mambo haya yaende kitaaluma. Hakuna sababu hili suala kuwa jinai, bali lishughulikiwe katika taratibu nyingine,” amesema.

By Jamhuri