Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

IMEELEZWA kuwa bado kuna vifungu vya sheria vinavyozuia uhuru wa habari na kuchangia waandishi wa habari kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Mhariri Mkuu wa gazeti la Jamhuri Jose Beda (kulia) akipokea flash yenye mapendekezo ya mabadiliko ya sheria za habari kutoka kwa Mwenyekiti Mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga,katika ofisi za gazeti la Jamhuri.

Hayo yameelezwa leo Agosti 15,2022 na Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga,katika ofisi za gazeti la Jamhuri wakati akizungumzia mchakato Mabadiliko ya Sheria ya Habari.

Amesema kuwa kuwepo kwa vifungu hivyo kumechangia waandishi wa habari kushindwa kutekeleza majukumu yao hivyo Serikali inapaswa kutunga sheria zitakazotoa uhuru kwa vyombo hivyo kutekeleza majukumu yake bila kuvunja sheria.

“Tunaendelea kuzungumzia suala hili la mabadiliko ya sheria ya habari kwa kuwa vipo vifungu vinavyowazuia na hata kuwanyima usingizi waandishi wa habari kwa kuwanyima uhuru wao na kushindwa kutekeleza majukumu ambavyo vinahitaji kufanyiwa marekebisho,’ amesema Makunga.

Makunga amesema kuwa pamoja na Serikali ya Awamu ya Sita kufungua milango kuhusiana na mabadilio ya sheria zinazoongoza tasnia ya habari nchini lakini ni wakati sasa wa kuchukua hatua na kuondoa hivyo vifungu ambavyo vimeonekana kuwabana waandishi wa habari ili wawe huru katika utekelezaji wa kazi zao.

Akizungumzia historia ya sheria ya vyombo vya habari nchini, Makunga amesema tangu awali, vyombo vya habari vilikuwa vikiendeshwa kwa sheria iliyoundwa mwaka 1979 – Sheria ya Magazeti.

“Sheria hii ilikuwa ikiongoza uandishi wa habari, utangazaji na namna gani ya kufanya, ilikuwa inasema ukiwa na kosa kwenye gazeti, anaweza kushtakiwa mwandishi, mhariri, mmiliki na mchapaji wa gazeti,” amesema.

Ameongeza kuwa hatua ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kupewa jukumu la kuangalia maudhui na kazi za habari kwa hili halijakaa sawa.

“Tunataka Idara ya Habari (MAELEZO) ibadilishwe jukumu lile, badala ya mambo yanayohusu tasnia ya habari kupewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO, lipewe Baraza Huru la Vyombo vya Habari kusimamia,” amesema Makunga.

Ameeleza kuwa, Baraza Huru la Vyombo vya Habari Huru linapaswa kuwa kama mabaraza ya taaluma nyingine akitoa mfano wa mabaraza ya madaktari na wanasheria yanavyoendeshwa.

“Fikiria kuwa umetoka nyumbani kuwa unakwenda ofisini na unapofika unapata taarifa ya gazeti kufunguwa kwa siku 90 hii inaumiza sana hivyo tunahitaji kuwa na Baraza Huru la Vyombo vya habari kusimamia,’ amesema Makunga.

By Jamhuri