Uzazi wa mpango na afya ya uzazi Tanzania

Na Stella Aron, JamhuriMedia

Huduma za kupanga uzazi ni moja ya afua mtambuka zinazopewa kipaumbele hasa katika huduma za kinga za afya. 

Huduma hizo za ni muhimu katika kufikia malengo makuu ya afya hasa katika afya ya uzazi na mtoto. Inachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya uzazi kwa takriban asilimia 44 kupunguza vifo vya watoto. 

Huduma hizo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa kaya na taifa, kuondoa umaskini na kupunguza njaa.

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya uzazi wa mpango ambayo huadhimishwa kila Septemba 26 ya kila mwaka dunia,Maranatha John (21), mkazi wa kijiji cha Mpuguzi mkoani Dodoma, anasema kuwa siku hiyo ni muhimu kwa familia kwa kuwa yeye imemsaidia kupanga familia kwa kushirikiana na mumewe.

“Siku ya maadhimisho ya afya ya uzazi kwani huwa ni muhimu kwa kuwa mumewe ndiye aliyeanza kusikia hizi habari za uzazi kwenye redio na akaniambia kumbe hata yeye anastahili kwenda kliniki na kupata elimu elimu hiyo.

“Sikuamini masikio yangu kwani awali alikuwa anikieleza kuwa yeye anataka watoto kumi kwa kuwa kwao wamezaliwa 9 hivyo haitakuwa njema kuzaa watoto pungufu ya hao.

“Niliamua kliniki katika zahanati ya Mpuguzi ambapo niliongea na nesi ndipo akanishauri nini cha kufanya na alinielekeza njia ya uzazi wa mpango kwa kutumia vijiti na nilifanya hivyo kwa siri kwa muda mrefu ili watoto niliwapa wapate nafasi ya kukua na kuwasomesha,’ anasema.

Anasema kuwa awali kabla ya mumewe kutoajua umuhimu wa uzazi wa mpango alikuwa akimueleza kuwa kila mtoto anapofikisha miaka miwili awe ana beba mimba nyingine ili kuhakikisha kuwa idadi ya watoto kumia wanafikia.

Maranatha anasema kuwa hali hiyo ilikuwa ikimpa ugumu kiasi kwamba alilazimika kwenda kwa rafiki yake na kumweleza na ndiye aliyemshauri kwenda kituo cha afya kupata ushauri.

“Bila shoga angu mama Dani naamini hadi sasa ningekuwa na watoto wasiokuwa na afya na ambao tusingeweza kuwalea ipasavyo kwani mbali ya kutumia njia ya uzazi wa mpango sasa hivi nina watoto wanne, wa kwanza yupo darasa tano, wapili darasa la tatu na wa tatu yupo shule ya awali na wanne ndiyo ananyonya ana mwaka na miez miwili,” anasema.

Anasema kuwa siku moja (mwaka jana Septemba) mumewe alitoka shambani ambapo wao ni wakulima wa zabibu akiwa amepumnzika nyumbani huku akiwa anasikiliza mpira ambapo siku hiyo Yanga ilikuwa ikicheza na Mbeya City na baada ya kuisha ndipo kipindi cha afya uzazi kiliendelea.

“Nashangaa baada ya muda aliniita ambapo mimi nilikuwa nje napika na kuniambia kuwa hakujua kama na yeye anatapaswa kwenda kliniki hivyo aliniambia kuwa siku ya kliniki nifuatane naye.

‘Kweli ilipofika Jummane nilikwenda naye klini na kumbuka siku hiyo hata foleni sikutakiwa kukaa kwani nesi alitupa elimu ya afya uzazi na kutakiwa kufuata uzazi wa mpango na alitueleza faida zitokanazo na uzazi hakika mumewe wangu siku hiyo hiyo alifuta kauli ya kutaka nizae watoto 10 akaniambia kuwa sasa atazaa watoto sita tu kwani wanatosha,” anasema.

Anasema kuwa tangu kuwepo kwa mabadiliko hayo hivi sasa wanaishi na mumewe kwa furaha kwani amekuwa mwalimu kwake kwa kumkumbusha kila mara anapotakiwa kwenda kliniki na kuzingatia uzazi wa mpango.

Hata hivyo takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), inaeleza kuwa vifo vya uzazi nchini Tanzania viliongezeka hadi vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 kutoka vifo 454 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2010. 

Elias Kweyamba ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, anasema asilimia kati ya 16 hadi 19 ya vifo vya uzazi vinatokana na utoaji wa mimba usio salama.

“Uzazi wa mpango husaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwani asilimia kati ya 16 hadi 19 ya vifo vya uzazi hutokana na utoaji wa mimba usio salama, elimu itasaidia kupunguza changa moto hii,” anasema 

Kwa sababu hiyo ipo haja ya Dunia husasani kwa nchi zinazoendelea kupata elimu sahihi ya njia za uzazi salama ili kuepuka mimba zisizotarajiwa ambazo mara nyingi hutolewa kwa njia hatarishi. 

Zawadi Joseph (26), mkazi wa Dodoma ambaye ni mama wa watoto 5 anasema kuwa elimu zaidi inahitajika hasa kwenye matumizi ya njia za uzazi wa mpango. 

Anasema hivi sasa hata afya yake si nzuri kutokana na kupata watoto mfululizo huku akibainisha kwamba malezi ya watoto kwa kufanya vibarua kwenye mashamba ya watu ni magumu. 

“Mimi nimewahi sana kuzaa baada ya kukatisha masomo nikiwa kidato cha kwanza na hii ndiyo imenisababishia hata mwili wangu kutokuwa katika hali njema kama wenzangu ingawa kwa sasa nimeingia kwenye uzazi wa mpango ingawa mumewe wangu hataki hivyo natumia kwa siri kwani sitarajii tena kubeba mimba,” anasema.

Anasema kuwa wanawake wengi hawana uelewa wa elimu uzazi wa mpango na ndio maana wamejikuta wakipata mimba zisizotarajiwa hivyo ni vyema elimu ya uzazi ikawafikia wanawake kwani ndio hupatwa na changamoto nyingi.

“Kweli kuna maudhi madogomdogo baada ya kutumia njia za kupanga uzazi ambapo hali hiyo huwalazimu baadhi ya akina mama kusitisha matumizi ya njia hizo na kuwasababishia kupata watoto wasiowatarajia ama kutoa mimba kwa njia hatarishi,” anasema.  

Akizungumzia changamoto za kupata mimba za karibu karibu Theresia Masanja (28), mwanakijiji kutoka Mpunguzi aliyekuwepo kwenye zahanati ya Mpuguzi mkoani Dodoma anasema mimba za mfululizo zilimfanya apoteze watoto wake wawili na kwamba baada ya kupata ushauri wa kitaalam wa njia za kisasa na bora za uzazi wa mpango amezifuata na sasa anaishi kwa furaha. 

“Nilipata mimba nikiwa na mtoto wa siku 40 kwa huku kijijini kwatu ni aibu nikatafuta mbinu za kienyeji za kutoa mimba. 

“Mtoto alikuwa na nyonya nikaelekezwa dawa nikanywa mimba ilishafikia miezi mitatu kumbe dawa ile niliyokunywa ni sumu kiumbe cha tumboni kilikufa na mimi hali yangu ikawa mbaya nilisafishwa kizazi huku nyumbani mwanangu mdogo aliugua na kwa kuwa hakunyonya hali ilikuwa mbaya akaletwa hospitali lakini haikuwa habati, mwanangu akafariki akiwa na miezi mitano. 

“Nilipata elimu na vipimo nikakubaliana na watoa huduma na sasa natumia njia ya kitanzi. Nimebaki na watoto wawili mkubwa ana miaka 12 na mdogo ni huyu wa mwaka mmoja na nusu,” anasema Masanja huku akitabasamu. 

Anazitaja njia nyingine za uzazi wa mpango anazozifahamu kuwa ni mipira ya kiume, sindano, dawa, kijiti na kufunga uzazi. 

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Mussa Mfaume anasema ofisi yake imefungua milango kwa mashirika binafsi kupeleka elimu ya uzazi wa mpango kwa wanaume ambao ni wadau muhimu kwa mustakabali ya afya ya mwanamke na watoto. 

“Licha ya kutoa kipaumbele kwa wanaume wanaokuja kliniki na wake zao kupata huduma kwa haraka bado elimu zaidi inahitajika ili suala la afya ya uzazi liwe jambo la kifamilia,” amesisitiza Dk.Mfaume 

Ozia Dominic ni mtoa huduma wa afya ya uzazi na uzazi salama, , anasema wanawake wengi wanajitokeza kupata elimu kuliko wanaume hivyo wanawahamasisha kuwapeleka waume zao. 

Hata hivyo tafiti mbalimbali za wataalam wa afya chini ya UNFPA zinaonesha kwamba zaidi ya wanawake na wasichana bilioni 1.8 wako katika kundi la umri wa uzazi lakini wengi wao wanakabiliwa na vikwazo ambavyo ni ukosefu wa taarifa sahihi na huduma bora za kupanga uzazi kutoka kwa watumishi wenye utaalam. 

Nchini Tanzania asilimia 32 tu ya wanawake walio katika umri wa uzazi wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango huku asilimia 22 wakiwa na mahitaji ambayo hayajafikiwa. 

Kwa kuzingatia kanuni zilizopo zinazowaweka wasichana kwenye ngono na ndoa za utotoni, asilimia 27 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 19 na 15 ni wajawazito au wameanza kuzaa. 

Matokeo yake, wanakabiliwa na hatari kubwa za kuharibika kwa mimba, utoaji mimba usio salama, aina nyingine za magonjwa ya uzazi ikiwemo saratani na vifo kutokana na matatizo ya ujauzito na uzazi.