Vidonda vya tumbo na hatari zake (15)

Katika sehemu ya 14 ya mfululizo wa makala haya, Dk. Khamis Ibrahim Zephania alieleza sababu za kutoka damu na saratani ya tumbo. Sasa endelea kumfuatilia zaidi…

 

Saratani ya tumbo ni aina ya saratani ya pili kubwa duniani. Hatari ya ugonjwa hutegemea ni kwa kiwango gani madhara ya utandotelezi (mucus membrane) yamekuwapo kabla ya H. pylori.

 

Madhara yanaweza kupimwa wakati wa kufanya endoscope. Maambukizi ya H. pylori husaidia viashiria vya saratani vinavyoitwa atrophic gastritis. Huonekana kuanza wakati wa utotoni.

 

Saratani huweza kujitokeza kupitia tumbo, huwa na uvimbe sugu na hupoteza vidoa vya tezi ambavyo hutema protini na asidi. Asidi hukinga dhidi ya visababisha kansa (carcinogens), vitu ambavyo huleta mabadiliko ya kikansa katika seli.

 

Au seli mpya huziba pengo la seli zilizoharibika, lakini hazizalishi asidi ya kutosha kukinga visababishi kansa. Baada ya muda, seli za kansa huanza kutokea na kujizidisha ndani ya tumbo.

 

Pindi maambukizo ya H. pylori yanapoanza ukubwani, huweka hatari ndogo ya kansa, kwa sababu huchukua miaka mingi viashiria kansa kutokea, na mtu mzima huweza kupoteza maisha kwa sababu nyingine.

 

Watu wenye vidonda vya duodeni vilivyosababishwa na H. pylori huonekana kuwa na hatari ndogo sana ya kansa ingawa wanasayansi hawajui ni kwa nini. Inafikiriwa inaweza kuwa kwamba H. pylori wanaoathiri duodeni ni tofauti na wanaoathiri tumbo. Au kiwango kikubwa cha asidi kinachotokea katika duodeni kinaweza kusaidia kuzuia kusambaa kwa bakteria katika maeneo muhimu ya tumbo.

 

Tafiti pia zinasema H. pylori anaweza kuchangia kutokea kwa saratani nyingine ikiwa ni pamoja na saratani ya kongosho na MALT lymphoma, ambayo kwa kawaida huanza katika maeneo ya mwili mahala ambapo kuna uvimbe wa muda mrefu, kutokana na kuingia wadudu au hali ya kinga  inayoathiri eneo hilo. MALT Lymphoma ni kansa ya B-Cells. Kwa kawaida huwaathiri watu wenye umri mkubwa wa miaka 60.

 

VIDONDA VYA TUMBO KWA MAMA WAJAWAZITO

Baadhi ya wanawake ambao ni wajawazito wanaweza kupata vidonda vya tumbo kabla ya ujauzito au baada ya ujauzito. Dalili za mara kwa mara za H. Pylori na matatizo ya viashiria vya vidonda vya tumbo, huonekana kupungua kwa wanawake wengi wajawazito labda kama dalili za vidonda vya tumbo ni kali sana.  Madaktari wengi huepuka kutumia njia ya endoscope kuchunguza dalili na kutambua chanzo kwa wajawazito.

 

Wanawake ambao wana historia ya vidonda vya tumbo ambao wamekuwa wajawazito wanaweza kuendelea na matibabu na dawa wakati wa ujauzito, kama ni muhimu sana kufanya hivyo; baadhi ya dawa za hospitali ni salama kwa mama mjamzito, lakini nyingine si hakika kama ni salama.

 

Tunatumbua kwamba dawa huweza kutuliza na kuponya magonjwa, lakini pia huweza kuleta madhara makubwa hata kifo kama zitatumiwa vibaya. Kwa mama mjamzito, madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya dawa yanaweza kusababisha mtoto kuzaliwa kilema, mtoto kufia tumboni na kifo kwa mama.

 

Dalilli za kiungulia na dalili nyingine za acid reflux huonekana kuongezeka na wanawake wengi wanaweza kutafuta matibabu ya dawa kwa ajili ya dalili hizi ukizingatia antacids pekee haziwezi kusaidia kupunguza tatizo.

 

Hata hivyo, wataalamu wengi wanaamini kwamba antacids zinapaswa kuepukwa wakati wa majuma 10 ya ujauzito.

 

Licha ya kwamba dalili za vidonda vya tumbo hutoweka wakati wa ujauzito kwa wanawake wengi, baadhi ya wanawake hulalamika maumivu ni makali. Hii kwa kawaida hutokea kwa wanawake ambao maumivu ya vidonda vya tumbo yalikuwa makali walipokuwa si wajawazito.

 

Katika hali hizi, baadhi ya dawa asilia ni bora zaidi kutumia kuzuia asidi kuingia tumboni hadi mama mjamzito atakapojifungua, hivyo anaweza kuendelea na dawa ambazo hazina madhara kama ni muhimu kufanya hivyo.

 

Asidi ya tumbo haisababishi vidonda vya tumbo peke yake, bali pia husababisha dalili za vidonda vya tumbo – kuchoma, kichefuchefu, kutapika n.k. Kwa kufahamu hivyo, mama mjazito anaweza kuchagua kula vyakula vinavyozuia asidi kuingia tumboni hadi wakati wa kujifungua.

 

Hakuna mwongozo maalum juu ya vyakula vinavyozidisha vidonda na vyakula au vinavyosaidia uponyaji. Hii ni kwa sababu akina mama hupata matokeo tofauti katika vyakula. Kuna vyakula ambavyo baadhi ya akina mama huhisi kichefuchefu na wengine hapana.

 

Hata hivyo, vyakula vinavyodhaniwa kwa sehemu kubwa vinaweza kusababisha kiungulia vinapaswa kuepukwa. Vyakula hivi ni pamoja na vyakula vyenye mafuta mengi, caffeine. Vyakula vya asidi, matunda ya striki vinaweza pia kuongeza uzalishaji wa asidi ambayo matokeo yake ni kiungulia. Pia vitu kama sigara na pombe lazima viepukwe.

 

Kwa kuwa vidonda vya tumbo huonekana kuzalisha dalili chache pindi tumbo linapokuwa halina kitu, itakuwa bora zaidi kula mlo mdogo mdogo ili chakula kiendelee kukaa tumboni.

 

Pia epuka kula kupita kiasi kwa sababu huchochea uzalishaji wa asidi nyingi. Pia, chakula kinapokuwa kingi tumboni hulifanya tumbo kujitandaza sana, hivyo kuchokoza vidonda.

 

Mama mjamzito aepuke maziwa. Tunaweza kuwa tunasikia maziwa hutuliza na kufunika vidonda vya tumbo visichomwe na asidi, hilo ni kweli. Lakini, kwa hakika kama maziwa yatakuwa mengi yanaweza kusababisha uzalishaji mwingi wa asidi kwa mujibu wa tafiti za kitaalamu za hivi karibuni.

 

Itaendelea