Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dodoma

Wizara ya Afya kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI hadi sasa imeweza kusambaza vifaa vya mtu kujipima mwenyewe maambukizi ya Virusi vya UKIMWI zaidi ya Mil. 1.6 kuanzia Mwaka 2021 nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo kwenye kilele cha Mdahalo wa Kitaifa wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ambapo Mgeni rasmi alikua ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

Waziri Ummy amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kuongeza nguvu za kusambaza vifaa hivyo vya watu kujipima wenyewe Virusi vya UKIMWI ili kuweza kutambua hali zao wenyewe na kwa haraka kuhusu ugonjwa huo.

Waziri Ummy amebainisha kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kupanua wigo wa vituo vya kupima na kutoa huduma za matunzo (CTC) kwa watu wenye UKIMWI ambapo hadi sasa tuna vituo 8,529.

“Nitoe rai kwa watu wote wanaoishi na VVU kuzingatia matumizi sahihi na endelevu ya dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI ili kuweza kujilinda wao wenyewe lakini pia kuwalinda wengine” amesisitiza Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa huduma za kupima, tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU hapa nchini ili vituo vyote vinavyotoa huduma za Afya viwe pia vituo vya kupima na kutoa matunzo (CTC) kwa 95% ifikapo Mwaka 2025.

Aidha, Waziri Ummy amesema chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia, Serikali itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vitendanishi kwaajili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na kuendelea kufuatilia taarifa zote kuhusu uwepo wa dawa mpya ambazo ni bora zaidi.

Mwisho, Waziri Ummy amelipongeza Baraza la Taifa la watu wanaoishi na VVU Tanzania (NACOPHA) kwa kuanzaa mdahalo wa kuadhimisha Miaka 20, “Sekta ya Afya inatambua mchango wao mkubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI”. Amesema Waziri Ummy.

By Jamhuri