JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

Idara ya Upelelezi nchini Afrika Kusini imetangaza kuwa imewagundua watu 12 waliohamasisha maandamano yaliyosababisha vurugu na uporaji katika majimbo mawili makubwa nchini humo.

Vurugu hizo zilianza baada ya Mahakama ya Katiba kumhukumu rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma, kifungo cha miezi 15 gerezani baada ya kumtia hatiani kwa kuidharau mahakama.

Taarifa za upelelezi zinaonyesha kuwa vurugu hizo ziliandaliwa na kuhamaishwa na watu waliolenga kuidhoofisha serikali na kufungwa kwa Zuma kulitumiwa kama kisingizio tu.

Majimbo mawili, KwaZulu-Natal ambalo ndiko nyumbani kwa Zuma na Jimbo la Gauteng, ndiyo yaliyoathirika sana na vurugu hizo zilizohusisha uporaji na uharibifu wa mali katika biashara za  kampuni na watu binafsi.

Inadaiwa kuwa vigogo hao 12 walitumia mitandao ya kijamii kupanga na kuhamasisha vurugu hizo. Hilo liliwezekana kwa kuwa watu wengi nchini humo hivi sasa wanatumia mitandao hiyo.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa raia wapatao milioni 38 wa Afrika Kusini wanatumia internet na milioni 25 wanatumia mitandao ya kijamii.

Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita watu zaidi ya 79 waliripotiwa kufariki dunia katika vurugu hizo huku takriban watu 1,354 wakikamatwa.

Serikali nchini humo ililazimika kutumia jeshi la ulinzi kuongeza nguvu katika kukabiliana na vurugu hizo baada ya Jeshi la Polisi kuzidiwa.

Vurugu hizo zilianza siku kadhaa huko KwaZulu-Natal ambako magari 35 yalichomwa moto na waandamanaji. Vurugu hizo zikasambaa na badala ya kupinga kufungwa kwa Zuma waandamanaji wakaanza kuvamia maduka na biashara za watu, kuharibu mali na kupora.

“Watu hawa (12) wana uzoefu wa kufanya operesheni,” alisema Naibu Waziri wa Ulinzi wa jimbo hilo, Zizi Kodwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita.

Kituo cha News24 kiliripoti kuwa mkuu wa idara ya ukachero katika kipindi cha urais wa Zuma na balozi wa zamani wa Afrika Kusini nchini Japan, Thulani Dlomo, ni mmoja wa watu 12 wanaodaiwa kuandaa na kuhamasisha vurugu hizo.

Baada ya siku kadhaa za vurugu, jeshi liliingizwa mitaani baada ya Jeshi la Polisi kuzidiwa na kwa kiasi fulani likafanikiwa kuzima vurugu hizo katika sehemu kubwa.

Takriban wanajeshi 25,000 waliingia mitaani wiki iliyopita.

Wakati hali ikionekana kutulia katika Jimbo la Gauteng, hali haikuwa shwari Durban, makao makuu ya KwaZulu-Natal. Meya wa Jiji la Durbn, Mxolisi Kaunda, alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa vuguru hizo zilikuwa zimesababisha hasara ya rand bilioni 15 hadi kipindi hicho.


Katibu Mkuu wa Chama cha ANC aliyesimamishwa, rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma na Mkuu wa Idara ya Operesheni Maalumu wa zamani, Thulani ‘Silence’ Dlomo. 

By Jamhuri