Vyombo vya habari ni chuo cha maarifa

Vyombo vya habari (mass media) ni njia ya
mawasiliano kati ya mtu na mtu, katika
kuhabarishana, kuelimishana na
kuburudishana. Iwe wakati wa kazi,
mapumziko au starehe. Ni njia ya kufikia
kupata maendeleo ya kiuchumi na kijamii
katika taifa lolote duniani.
Kila chombo (medium) kinafanya kazi kwa
maadili ya kazi, kanuni na weledi.
Kushirikiana na kingine katika kupokea na
kutoa taarifa mbalimbali katika mustakabali
wa maendeleo ya mtu au jamii.
Redio, magazeti, runinga, filamu, video,
vitabu, majarida, simu, teleksi na mitandao
ya kijamii ni vyombo vya habari. Vyombo
vyote hivi vinafanya kazi chini ya miundo,
sera na taratibu za utekelezaji wa masuala
ya habari katika kutimiza madhumuni na
malengo ya mamlaka zinazoendesha

vyombo hivi.
Ukiangalia utendaji kazi wa vyombo hivi,
utaona ni njia ya kupitisha au kusafirisha
mawazo, fikra au ujumbe kutoka upande
mmoja kwenda upande wa pili. Ni lazima
vipitishe ujumbe unaokusudiwa. Ni
matarajio ya mtumaji na mpokeaji habari,
elimu na burudani kujenga uhusiano
mwema.
Hapa ndipo penye uangalifu, ni aina gani ya
ujumbe unatumwa na unapokelewa kati ya
mtu na mtu. Ama sivyo vyombo hivi
vitatumika kwa madhumuni na malengo
mabaya badala ya mazuri.
Kitendo cha usafirishaji au upashanaji
habari, fikra, rai kwa njia mbalimbali
zikiwamo za vyombo vya habari ndiyo
mawasiliano yenyewe. Mawasiliano yapo ya
mtu na mtu, jamii na jamii na taifa na taifa.
Vyombo hivi ili viwe na sifa ya kupasha
habari havina budi kuwafikia watu wengi
sana kwa wakati mmoja. Watu wengi sana
katika istilahi ya habari ndiyo umma
(hadhira). Ndipo vinapokuwa vyombo vya
mawasiliano na umma. Katika mazingira
haya vyombo hivi vitumike kwa umakini.

Katika lugha rahisi na fupi kutamka
tunasema vyombo vya habari, kwa lugha ya
Kiingereza ni ‘Mass Media’

, vyombo hivi
vina uwezo na sifa za msingi kuwafikia watu
wengi sana, katika sehemu mbalimbali na
katika mazingira tofauti. Vilevile haraka
sana na kwa wakati mmoja.
Kwa sifa hizi, baadhi ya watumiaji
(wasikilizaji na wasomaji wa habari)
wanatumia vibaya vyombo vya habari: kwa
maana ya kinyume cha malengo na
madhumuni ya kuwapo kwa vyombo hivi.
Wanavitumia katika kujenga chuki, fitina,
kejeli, dharau na kadhalika.
Wakati mwingine bila hadhari, tafakuri na
uelewa wa taarifa, nao baadhi ya waandishi,
watangazaji na wasimamizi wa matangazo
wanajikuta wametumbukia katika
malumbano ya kisiasa na kijamii kupinga au
kukubali ujumbe unaopita katika vyombo
vyao.
Kushiriki kwao katika malumbano hujenga
taswira kwa umma kuona na kuamini
matangazo ya malumbano ya kejeli au
dharau ni moja ya sifa na adilifu ya vyombo
vya habari. Jambo ambalo si kweli na si

sahihi. Ni vema tukajitoa katika hili na
kuweka umma katika mazingira salama.
Hekima na busara iliyoje kwa viongozi,
umma na wanahabari wote nchini kuacha
kutumia tabia ya kutafuta malumbano ya
uhasama badala ya malumbano ya amani
na usalama. Tukumbuke kila mchuma janga
hula na wa kwao. Wa kwao wenyewe ndio
Watanzania, tutaangamia.
Vyombo vya habari si ukumbi wa mipasho,
si jukwaa la visanga na si kambi ya
mafunzo ya vita. Vyombo vya habari ni
mlango wa maarifa, ni chuo cha mafanikio
na ni bahari ya amani na usalama. Mungu
ibariki Tanzania, tubariki watoto wa
Tanzania.

Mwisho