New York, Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini,
Ri Yong-ho, ameonya kuwa hakuna namna
ambayo nchi yake itaharibu zana za nyuklia
wakati Marekani bado inaendelea kuiwekea
vikwazo.
Ri Yong-ho aliuambia mkutano wa Umoja wa
Mataifa unaoendelea jijini New York, Marekani
kwamba vikwazo hivyo vinapunguza imani kwa
Marekani.
Hivi karibuni Korea Kaskazini imerejea wito
wake wa kuitaka Marekani na Umoja wa
Mataifa kuondoa vikwazo hivyo na imeungwa
mkono na washirika wake wa karibu kutoka
China na Urusi.

Lakini uongozi wa Rais wa Marekani, Donald
Trump, unasema vikwazo hivyo vitadumu hadi
pale Korea Kaskazini itakapoharibu zana zake
za nyuklia.
Rais Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini,
Kim Jong-un, walifanya mkutano wa kihistoria
mwezi Juni, mkutano huo ulifanyika nchini
Singapore, ambapo Rais Kim aliahidi kuharibu
zana za nyuklia.
Waziri wa Mambo ya Nje, Ri,
anasema Marekani ilikuwa inasisitiza suala la
kuharibiwa silaha kwanza, sera ambayo
iliongeza idadi ya vikwazo.
“Bila ya imani kwa Marekani hatuwezi kuwa na
uhakika wa usalama wetu wa kitaifa, na katika
hali kama hiyo, hatuoni sababu ni kwa namna
gani tutaharibu silaha zetu kwanza.
“Imani kuwa vikwazo vinaweza kuchangia sisi
kusalimu amri ni ndoto,” alisema.

Kipi kimefanyika tangu mkutano wa
Singapore?

Makubaliano yaliyoafikiwa huko ni kwamba
Korea Kaskazini ingeharibu zana zake za
nyuklia, lakini hayakuwa na mwongozo au
muda au njia ya kuthibitisha mchakato huo.
Mwezi Agosti Rais Trump aliilaumu China
ambaye ni mshirika wa karibu wa Korea
Kaskazini kwa suala hilo kutokana na tofauti
zake za kibiashara na Marekani.
Hata hivyo mapema mwezi huu Kiongozi wa
Korea Kusini, Moon Jae-in, alifanya ziara ya
siku tatu nchini Korea Kaskazini – ikiwa ndiyo ya
kwanza kufanywa na rais wa Korea Kusini mjini
Pyongyang kwa miongo kadhaa.
Rais Moon anasema aliweza kuthibitisha
kujitolea kwa Kim Jong-un katika kuharibu zana
za nyuklia, pia alikuwa na nia ya kukutana tena
na Rais Trump hivi karibuni.
Kim pia aliahidi kuharibu eneo kuu la kufanyia
majaribio ya makombora.

Mwisho

By Jamhuri