Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

UJUMBE wa viongozi na wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari kutoka nchini Oman (OJA), wametembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kujifunza na kuona fursa za ushirikiano.

Ujumbe wa OJA uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa OJA, Salem bin Hamad Al-Jahwari chini ya uratibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) ambao ndio waratibu wakuu wa ziara hiyo.

Wakiwa UDSM ,waandishi hao walipokewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko wa Dk Doto Kuhenga na viongozi wengine wa chuo hicho.

Akizungumza na ujumbe wa OJA , Dk Kuhenga anaahukuru JOWUTA kwa kuwezesha ujumbe huo kutembelea chuo hicho kikongwe na kwamba hiyo ni fursa ya kushirikiana baina ya Tanzania na Oman katika nyanja kadhaa.

Dk Dotto aliwaeleza wanahabari hao historia ya chuo hicho tangu uhuru hadi sasa, mafanikio na malengo ya chuo hicho ambacho kina historia kubwa ya uhuru wa mataifa mengi barani Afrika.

Mkurugenzi huyo alikubaliana na hoja za kufungua milango ya ushirikiano kitaaluma hasa katika masomo lugha, uandishi wa habari na technolojia ya mawasiliano hasa Akili Unde (AI).

Wakiwa TBC wanahabari hao pia walipata fursa kutembelea kituo hicho na kupata maelezo ya harakati za TBC tangu uhuru hadi sasa lakini pia fursa za ushirikiano.

Makamu Mwenyekiti wa OJA, Salem amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa mengi ikiwemo kujua historia ya UDSM na TBC na kuahidi kuendeleza ushirikiano.

Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma aliwashukuru OJA kwa kufika Tanzania na kuahidi yale yote waliokubaliana katika hati za makubaliano yatatekelezwa.

Juma pia aliwataka wanahabari hao kwenda Oman kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini katika sekta kadhaa ikiwepo Utalii,Habari, Elimu,Miundombinu na biashara.

Viongozi wengine wa JOWUTA walioshiriki ziara hiyo ni Katibu Mkuu Seleman Msuya na Naibu Katibu Mkuu Said Mmanga.