Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Tabora

TUME ya Taifa ya uchaguzi imewataka wakazi wa Mikoa ya Tabora na Mara kujitokeza kwa wingi kwenye majaribio ya uboreshwaji taarifa za wapiga kura kwenye mfumo ili kufanikisha zoezi hilo kwa asilimia 100.

Wito huo umetolewa leo na Mjumbe wa Tume hiyo Balozi Omar Ramadhan Mapuri katika mkutano wa Tume na Wadau wa uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Amesema lengo la zoezi hilo ni kuvifanyia majaribio vifaa na mfumo wa uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura ili kuangalia ufanisi wake ikiwemo kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza ili kuzipatia ufumbuzi mapema kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi hilo nchi nzima.

Amebainisha kuwa zoezi hilo litahusisha uandikishaji raia wa Tanzania waliofikisha umri wa miaka 18 au zaidi na atakayetimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi Mkuu wa 2025.

Kundi jingine ni la wapiga kura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja kwenda jingine, waliopoteza au kadi zao kuharibika, wanaorekebisha taarifa zao na kuondoa walipoteza sifa za kuwemo katika daftari.

Mapuri amefafanua kuwa katika majaribio hayo Tume itatumia Mfumo wa Uandikishaji Wapiga Kura (Voters Registration System-VRS) ambao umewekwa katika kifaa cha Biometric Voters Registration-BVR ndogo chenye uzito wa kilo 15 kikiwa na vifaa vya kisasa tofauti na kile kilichotumika mwaka 2019 na 2020.

Ameongeza kuwa mfumo huo utatumika kuandikisha wapiga kura wapya, kuboresha taarifa zao, kuondoa kwenye daftari la kudumu waliopoteza sifa na kutoa kadi mpya kwa walipoteza au kuharibikiwa.

‘Majaribio hayo yanatarajiwa kufanyika mwezi huu kuanzia tarehe 24 hadi 30, 2023 katika kata za Ng’ambo (halmashauri ya manispaa Tabora na kata ya Ikoma katika halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara,’ amesema.

Amesisitiza kuwa zoezi hilo ni muhimu sana hivyo akawataka wakazi wa Mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi ili kuangalia ufanisi wa vifaa hivyo kabla ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2023.

Awali akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Tume hiyo, Mwenyekiti wa Kitengo cha Huduma za Kisheria Suleiman Mtibora alisisitiza kuwa wadau wa uchaguzi ni watu muhimu sana katika kufanikisha zoezi hilo ikiwemo kudumisha demokrasia, upendo, amani na utulivu wa nchi hivyo akawataka kutoa maoni yatakayosaidia kufanikisha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa.

Ameeleza sababu za majaribio hayo kufanyika katika kata hizo kuwa ni kutokana na ongezeko la watu, hali ya miundombinu ya mawasiliano, mazingira na muingiliano mkubwa wa watu ikiwemo nchi jirani kwa maeneo ya mipakani.

By Jamhuri