Na Elizabeth Joseph,JamhuriMedia,Arusha

WAKUFUNZI wa Mpango wa Uwezeshaji kupitia Ujuzi(ESP), unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Serikali ya Canada wametakiwa kutumia mafunzo wanayopewa katika kukuza uelewa kwa jamii katika masuala ya Haki za Binadamu,Jinsia na Uongozi kwa kuleta mabadiliko kwa wanawake nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia masuala ya Elimu Msingi na Ufundi Carolyne Nombo wakati akiongea na waandishi wa habari mkoani Arusha.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na walezi kutoka Vyuo sita vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs), wawakilishi kutoka Asasi za Kiraia shirikishi (AZAKI) sita na Maofisa Maendeleo ya Jamii (CDOs) kutoka Wilaya za Monduli, Kilwa Masoko, Kondoa, Morogoro, Muheza, na Singida.

Kushoto ni Stephen Kijazi Ofisa Programu wa Ubalozi wa Canada nchini akiwa na Katibu wa Kwanza wa Maendeleo ya Ukuaji na Uchumi Canada,Bw Christopher Duguid

Alisema kuwa mafunzo hayo yakitumiwa vizuri yatasaidia kuleta matokeo chanya katika kubadili Imani na uelewa wa jamii katika masuala ya Jinsia,kutambua na kuelewa haki za Binadamu hasa kwa upande wa Wanawake pamoja na kuleta usawa katika masuala ya kiuchumi na maendeleo katika jamii nchini Tanzania.

“Kwa pamoja tutapata fursa ya kubadilisha maisha ya wanawake na kuondokana na vikwazo vya ajira,kujiajiri na ujasiriamali kwa kazi muhimu na msaada wa vyuo vya Maendeleo ya Wanachi Tanzania pamoja AZAKI..…….

“Kundi hili ni muhimu katika jamii zao lina uwezo wa kubadilisha maisha ya wanaume na Wanawake,wavulana na wasichana nchini Tanzania kutokana na nafasi zao za kimkakati katika jamii na mamlaka yao ya kuleta mabadiliko ya Kijamii ndani ya nchi”alisema Bi Nombo.

Aliongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itahakikisha inawawezesha wanawake kufuata fursa za kiuchumi na Kijamii,kuendelea mazingira wezeshi kwa mahusiano ya usawa wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kusaidia kuunda nafasi salama kwa Wanawake katika Jumuiya zao.

Naye Stephen Kijazi ambaye ni Ofisa Programu kutoka Ubalozi wa Canada nchini Tanzania alieleza kuwa Serikali ya Canada inajivunia kuunga mkono ukuaji wa mpango wa Uwezeshaji kupitia Ujuzi(ESP) na kuongeza kuwa Canada itaendeleza uwekezaji katika maendeleo katika Elimu,Usawa wa kijinsia na Ukuaji wa kiuchumi.

Kwa upande wake Mshauri wa Mradi kutoka ESP katika masuala ya Kijinsia Bi Alice Mumbi alisisitiza umuhimu wa kufikia malengo ya Mradi huo ili kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kutoa fursa sawa kwa Wanawake,wanaume, wavulana na wasichana ili kupata mabadiliko chanya.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia

Mumbi aliongeza kusema kuwa mradi huo unalenga kuwafikia wanajamii 2,400 ambao watashiriki katika shughuli za usawa wa kijinsia na uhamasishaji wa haki za Binadamu huku jumla ya Wanawake na wasichana 480 wakitarajia kumaliza mafunzo mafupi ya ustadi unaozingatia Jinsia ambayo alisema yanatolewa na AZAKI katika Jamii.

Hata hivyo mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Mary Laizer kutoka Shirika la Maasai Stoves & Solar lililopo Wilaya ya Monduli mkoani Arusha alishukuru kupata mafunzo hayo na kusema yatasaidia kupunguza ukatili wa kijinsia katika jamii wanazotoka kwakuwa watakuwa mabalozi katika kupinga ukatili dhidi ya watoto na Wanawake ikiwemo Ndoa na mimba za utotoni.

ESP ni progamu ya miaka 7(2021-2028) inayotekelezwa na Vyuo na Taasisi za Canada(CICan)kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Tanzania (MoeST) kupitia Idara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi huku lengo kuu ikiwa ni kuimarisha njia mbadala za Elimu,Ajira, Ujasiriamali kwa Wanawake na Wasichana.