Na Albano Midelo, JamhuriMedia,Tunduru

Wakulima wa ufuta katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wameingiza zaidi ya shilingi bilioni 10.5 baada ya kuuza tani 1626 za ufuta katika minada mitatu iliyofanyika kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani,

Hayo yamesemwa na Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Gorge Bisani katika mnada wa tatu wa ufuta uliofanyika katika kijiji cha Namiungo Tarafa ya Nakapanya ambapo wakulima waliridhia kuuza ufuta kilo shilingi 3,808,jumla ya kilo milioni moja na elfu sitini zimeuzwa.

Amesisitiza kuwa tani za ufuta zilizouzwa na wakulima katika minada mitatu iliyofanyika hadi sasa zinaweza kuvuka malengo ya kuzalisha ufuta kwa mwaka huu ambayo yalikuwa ni tani 3,000 hivyo uzalishaji unaweza kufikia zaidi ya tani 4,000 za ufuta kwa kuwa ufuta bado mwingi kwa wakulima.

Afisa Ushirika wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Gorge Bisani akizungumza na wakulima wa ufuta katika kijiji cha Namiungo tarafa ya Nakapanya ambako umefanyika mnada wa tatu za zao la ufuta na wakulima kuuza ufuta tani zaidi ya 1000 kwa kilo moja shilingi 3,808

Bisani amesema zao la ufuta linaonesha lina manufaa makubwa kwa wakulima na kuwa ni zao mbadala kwa korosho ambapo kwa mwaka huu bei ya ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani imekuwa kivutio kwa mkulima.

Ameyataja maeneo yanayoongoza kwa uzalishaji wa ufuta wilayani Tunduru kuwa ni Marumba, Lukumbule na Mtesa na kwamba zao la ufuta limebadilisha Maisha ya wakulima ambapo wakulima wengi wameweza kujenga nyumba za kisasa na kusomesha Watoto wao.

“Ukitaka kujua mchawi wa zao ni bei,bei inapokuwa nzuri sokoni inawashawishi wakulima kurudi shambani na kuongeza uzalishaji zaidi,naamini mwakani uzalishaji wa zao la ufuta utaongezeka maradufu’’,alisisitiza Bisani.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) Musa Manjaule akizungumza kwenye mnada wa tatu wa zao la ufuta uliofanyika katika Kijiji cha Nimiungo,alisema Katika mnada huo jumla ya Kampuni 11 zilishindanishwa ambapo kampuni saba zilifanikiwa kununua ufuta tani zaidi ya 1000 kwa bei ya wastani ya shilingi 3,808 kwa kilo.

Amesema bei ya ufuta ya shilingi 3,808 katika mnada wa tatu bado ni nzuri kwa wakulima wa Tunduru ukilinganisha na minada iliyofanyika katika mikoa ya Lindi na Songwe ambapo wakulima wameuza kilo kwa shilingi 3,700.

baadhi ya magari yakisafirisha zao la ufuta kutoka ghala kuu la Chama Kikuu cha Ushirika TUnduru (TAMCU) ambapo hadi sasa wakulima wameweza kuuza tani 1626 za ufuta katika minada mitatu na kuwaingizia shilingi bilioni 10.5

Hata hivyo Manjaule ametoa rai kwa wanunuzi wa ufuta katika mnada ujao waendelee kuongeza bei ya ufuta kwa kuwa wakulima wanafanya kazi katika mazingira magumu hivyo bei ya juu itatoa tija kwa mkulima kuongeza uzalishaji.

Rashidi Musa Mkulima wa ufuta katika Kijiji cha Namiungo akizungumza baada ya kufanyika mnada huo ameipongeza serikali kwa kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani,hata hivyo ameiomba serikali kukopesha wakulima dawa za kuongeza ubora wa ufuta.
Ally Omary Mkulima wa Namiungo amesema bei ya ufuta kwa mwaka huu,inatio moyo na kuwafanya wakulima ambao hawakulima mwaka huu,kujiandaa katika msimu ujao kulima ufuta kwa wingi.

Huu ni mnada wa tatu wa ufuta kufanyika katika wilaya ya Tunduru ambapo katika mnada wa kwanza uliofanyika AMCOS ya Lukumbule wakulima waliuza ufuta kilo shilingi 3,822 na katika mnada wa pili uliofanyika AMCOS ya Marumba wakulima waliuza ufuta kilo 3,895.