Walimu saba na wafanyabiashara wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu likiwemo la kuvujisha mtihani wa Taifa wa darasa la saba mwaka 2022.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo leo Oktoba 19,2022 na wakili wa Serikali Mwandamizi Nassoro Katuga imewataja washtakiwa hao kuwa ni Patrick Chawawa, Theresia Chitanda, Elinami Sarakikya, Joyce Nkomola , Lloyd Mpande, Olomy Odongo ,Docras Muro na Alcherous Malinzi.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Pamela Mazengo, imedaiwa,kati ya Oktoba 2 hadi 12, mwaka huu, jijini Dar es Salaam washtakiwa, walisambaza mtihani huo kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp na Telegram na kusababisha mtihani huo kuvuja kwa watu ambao hawakuwa na mamlaka ya kuusimamia.

Imeendelea kudaiwa kuwa katika tarehe hizo hizo Jijini Dar es Salaam mshitakiwa Malinzi alitengeneza nyaraka za uongo kuonesha kama mtihani wa Taifa wa darasa la saba wa somo la Uraia, Maadili na Maarifa ya Jamii kuwa mitihani hiyo ni ya halali na umetolewa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), wakati akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo washtakiwa wamekana kutenda makosa hayo na ni mshtakiwa mmoja tu ‘Mpande’ ndiye alifanikiwa kutimiza masharti ya dhamana huku wengine wote wakirudishwa mahabusu.

Mahakama imewataka washtakiwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh.Milioni tano

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika hivyo wameiomba mahakama kuipangia tarehe nyingine kwa ajali ya kutajwa ambapo imeahirishwa hadi Novemba 2, mwaka huu.

By Jamhuri