Walivyojipanga kuihujumu SGR

*Waibua hoja zilizokufa wakati wa Rais Magufuli, masilahi binafsi yatangulia

*Mawaziri, makatibu wakuu wameelewa, watendaji wapingana na sheria ya ununuzi

*Mkono wa Kenya watajwa katika vita ya biashara ya reli kubeba mizigo ya majirani

*Yadaiwa kuna kampuni zimejipanga kushinda zabuni zikwamishe ujenzi Tanzania

Na Mwandishi Wetu

Baada ya wiki iliyopita kuchapisha habari za jinsi baadhi ya wanasiasa na watendaji walivyojipanga kuhujumu ujenzi wa reli ya kisasa katika kipande cha 3 & 4 cha kutoka Makutupora – Tabora – Isaka, sasa ni rasmi yameibuka makundi yanayoonyesha sura halisi ya kile yanachokipigania kuwa ni kuhujumu ujenzi wa reli ya SGR, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Makundi haya yamekuwa na mjadala mzito katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari, yakisisitiza kifuatwe kifungu cha 64(1) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni ya 149(1) ya Mwaka 2013 ya sheria hiyo, ambavyo kwa pamoja vinataka kutangaza zabuni kupewe “kipaumbele” katika miradi ya kitaifa. Wenye taarifa za ndani wanasema kundi hili linatumia kifungu hiki kwa masilahi binafsi.

Hata hivyo, hawataki kutumia Kanuni ya 161(c) ambayo inasema bayana kuwa inaruhusu kuwapo mzabuni mmoja iwapo faida za kutumia mzabuni mmoja (single sourcing) ni kubwa kuliko kuitisha zabuni. 

“Sababu za msingi zipo na zisizotiliwa shaka. Mwanzo tulikuwa tunapata taarifa tunaziona si za msingi, kumbe hawa watu wamejipanga. Hawakuthubutu kuyafanya haya wakati wa Rais [John] Magufuli, sasa amefariki dunia wanataka kurejesha mwendo wa kuruka kupiga fedha ndefu, hili halikubaliki,” amesema mtoa habari wetu.

Ukiacha hilo, Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA) katika barua kadhaa ilizowasiliana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaungana na Bodi ya Zabuni ya TRC kupingana na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, anayependekeza kuwa kwa masilahi mapana ya taifa kipande cha 3 & 4, kitumie utaratibu wa kumpa kazi mzabuni mmoja.

“Hapa utaona Kadogosa yuko sahihi. Mwaka 2016 ilitangazwa zabuni ya Lot 1, zikaomba kampuni 40. Ilipofika muda wa kurejesha zabuni ilirudisha kampuni moja tu ya Yapi Merkezi kama mlivyoandika wiki iliyopita. Kampuni hizi zote ambazo hazikurudisha zilikuwa za China. Tulipata mawasiliano na mazungumzo yao, walikubaliana wasirudishe zabuni nchi yetu itikisike, twende kuwabembeleza waje kutujengea reli.

“Ukumbuke walifanya hivyo, baada ya awali kuleta benki ya kwao ikasema ingelikopesha taifa letu Sh trilioni 7.6 kwa ajili ya ujenzi wa reli (Julai 20, 2016). Kampuni za kwao zilipojitoa, hii benki nayo ikajitoa katika kutukopesha. Lot 2, nayo walifanya hivyo hivyo. Ziliomba kampuni 27, kampuni 26 kutoka China zikajitoa, tukabaki na Yapi Merkezi. Rais Magufuli akasema waache, hatutishiki, ipo siku watatamani kuja kujenga hapa kwetu.

“Lot ya 3 zilijitokeza kampuni 7. Kampuni 5 kutoka China hazikurejesha zabuni. Rais Magufuli alikuwa amesema hata hawa CCECC/CRCC JV tusiwape wanaweza kuwa wameweka bei ya chini kuwatisha Yapi Merkezi, maana bei si kigezo pekee cha kushinda zabuni. Inaangaliwa na uwezo wa kampuni kifedha na mambo mengine yakiwamo ya ubora wa kazi na usalama wa nchi. Mjadala ulikuwa mkali, ila mwisho akasema basi tuwape tuwajaribu. Tumemaliza miezi 9 sasa kwenye mkataba na hizi kampuni, hawajafikia hata asilimia 10 ya kazi waliyopewa.

“Mwaka 2015 mtakumbuka kampuni moja kutoka China iliingia mkataba wa kimagumashi na Tanzania kuwa ingejenga reli kwa kilomita moja dola milioni 6.2 sawa na Sh bilioni 14.26. Reli yenyewe ilikuwa spidi 80 na ni analogue. Walioingia mkataba huo wako mahakamani hadi sasa. Januari, 2021 kampuni moja kutoka China ilishusha bei na kusema itajenga kwa wastani wa dola milioni 3.9 kwa kilomita moja ya reli, karibu Sh bilioni 8.9. Ikapewa. Wasichojua wananchi ni siri kubwa.

“Kampuni hiyo hiyo inayojenga kwa dola milioni 3.9 kwa kilomita, katika mazungumzo mapya inataka kujenga kilomita moja kwa dola milioni 6.5 sawa na Sh bilioni 15.95 kwa Lot 3 na 5. Imeleta bei zilizopakwa rangi za dola milioni 5.7 sawa na Sh bilioni 13.11, lakini katika gharama hizo hakuna VAT 18%, hakuna gharama za kujenga vituo kama Tabora, hakuna gharama za mafunzo, gharama za maeneo ya kuteketeza taka na mambo mengine mengi.

“Lakini mbaya zaidi, tuna uzoefu sasa. Kampuni nyingi za China zinaleta bei ndogo wakati wa kuleta zabuni. Mkiisha kumpa zabuni anaanza kazi, kisha anaanza kuleta gharama mpya nyingi tu wanazoziita variation (tofauti ya gharama halisi na zilizopo kwenye mkataba). 

Nenda Busisi (daraja la Kigongo), Ubungo Interchange, angalia mikataba mbalimbali ya barabara jinsi wanavyojenga na kuleta variation cost kubwa.

“Unakuta mkataba ni Sh bilioni 20 kwa mfano, lakini hadi mnamaliza mnajikuta mmemlipa Sh bilioni 45. Unajiuliza,  ilikuwa na faida gani kumkatalia aliyekuwa wa pili akiwa na gharama ya Sh bilioni 30, tukampa huyu wa Sh bilioni 20 ambaye tumeishia kumlipa Sh bilioni 45? Tumejifunza kwa njia ngumu. Tunao wataalamu wetu wenye ujuzi wa hali ya juu katika negotiation (majadiliano) tuainishe gharama halisi, tuzipe kampuni zenye uwezo na miradi ijengwe na kuisha kwa wakati,” kimesema chanzo chetu.

Alipoulizwa juu ya hoja iliyotolewa na PPRA kupitia barua ya kwenda kwa TRC kuwa mchakato wa zabuni umesaidia nchi kuokoa dola 1,030,068,831.21 sawa na Sh trilioni 2.37 kwa kuipa zabuni Kampuni ya CCECC/CRCC JV, akasema: 

“Wewe tafuta hizo Lot 3 na 4 wanataka kuzijenga kwa shilingi ngapi. Si wamewasilisha maombi wote? Wewe uliza tu. Yapi wamekuwa wanajenga kwa dola milioni 4.07 sawa na Sh bilioni 9.36, uliza hawa wanataka kujenga kwa shilingi ngapi? Wasiwasi uliokuwapo juu ya kushusha bei wakati wanapewa hii zabuni, tayari umedhihirika. Hili la bei tumekwisha kuwafahamu, tunasubiri la kutokamilisha ujenzi kama nalo lipo. Niulize swali hili ukiisha mwaka mmoja tangu wamepewa mradi,” amesema.

Mmoja wa mawaziri anayelifahamu vizuri suala hili ameliambia JAMHURI: “Kwanza tunapaswa kufahamu nani anayetaka kutukopesha fedha za ujenzi huu. Si unaona? Kuwait wakitoa fedha za maji kama ule mradi wa maji Moshi, wanazipa zabuni kampuni zao. India nao vile vile. China ndiyo usiseme. Japan utaona JICA ndiyo wanaojenga, kwa hiyo sitashangaa tukipata mkopeshaji kutoka China, japo tuombe yasitukute yaliyowakuta Wakenya, kwa hakika itajenga kampuni ya Kichina. Fedha zikitoka Ulaya, basi hakika ujue hata mjenzi atatoka Ulaya. Hili ni la kawaida tu.

“Hizi fedha zinazokuja kama mikopo kwa njia ya misaada zinalindwa na kifungu cha 4(1)(b) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma kinachosema mtoa msaada asikilizwe kwanza anataka nani ajenge. Achana na hizo hadithi kuwa tunajenga kwa hela zetu. Ni fedha zetu ndiyo, ila kwa njia ya mkopo. Mkopo wenyewe unakuja kama msaada, hivyo tutalipa baada ya kujenga. Sasa akikwambia mtu ni fedha zetu, mwambie ndiyo. Ila muulize tunazo kwenye akaunti? Akikujibu, unipigie simu.”

Chanzo kingine cha uhakika kimeliambia JAMHURI kuwa katika ngazi ya mawaziri na makatibu wakuu wamelizungumza suala hili na wakakubaliana fedha zitatoka wapi na kwa nini ipewe kampuni iliyosimama pamoja na nchi wakati nyingine zimeisusa Tanzania. 

“Wewe fikiria zimeomba kampuni 40, 39 zote kutoka China zikajitoa. Yapi Merkezi, akabaki. Zikafanya hivyo Lot 2 na Lot 5 nayo ni kama zilijitoa zikaiacha moja ‘kutest zali’.

“Leo zimepata wapi ghafla mapenzi ya kuja kutujengea reli? Ile benki iliyogoma kutoa hela, imebadili msimamo? Si tutawapa zabuni watuache solemba? Tupambane tumalize reli hii ifike Mwanza kwanza, kama ni reli za kujenga nchi hii ndipo imeanza. Kuna ya Tabora – Kigoma, Mtwara – Mangaka, Rukwa – Tunduma – Ruvuma – Lindi – Dar es Salaam. Tutajenga Tanga – Kilimanjaro – Arusha hadi Musoma. Hii yote ni miradi.

“Lakini jambo jingine, nadhani umeusikia mgogoro wa Ufaransa na mataifa ya Marekani na Uingereza katika mkataba wa ujenzi wa nyambizi (submarine) zenye thamani ya dola bilioni 66 sawa na Sh trilioni 151.8 za Tanzania. Mkataba huu walianza kuzungumza kwa siri mwaka 2016, miaka 5 baadaye ukawaponyoka. Hukusikia mamlaka zao za ununuzi zikipiga kelele. Zinaungana na serikali zao kwa masilahi mapana ya taifa. Tulifanya hivyo katika bomba la mafuta ghafi la Hoima, Uganda hadi Tanga.

“Kuna mambo tunapaswa kukomaa kama nchi. Yapi Merkezi sisemi wapewe kama wana bei kubwa, lakini uhalisia wana vifaa vyote, wamekaribia kumaliza lot 1 & 2 za mwanzo, na kwa uzoefu mchakato wa mkataba wa ununuzi unachukua si chini ya mwaka mmoja kuukamilisha. Badala ya kuingia nao mkataba Novemba au Desemba, mwaka huu wakaanza kazi hii itakayochukua miezi 48, tunataka kuingizana kwenye nyimbo za PPRA.

“PPRA wafahamu kuwa hawapo kusimamia baadhi ya vifungu vya sheria na kanuni, huku wakivipuuza baadhi ya vifungu visivyotimiza matakwa yao. Sheria inaruhusu njia zote mbili. Kuitisha zabuni ukashindanisha wazabuni au kutafuta mzabuni mmoja (single sourcing) mwenye sifa, uzoefu na gharama halisi.

“Mimi nadhani mawaziri wanaosimamia hizi mamlaka watazungumza na watendaji wao, wasiyumbishe nchini. Vifungu vyote vya Sheria na Kanuni vina nguvu sawa. Tumetangaza huko nyuma yaliyotukuta tumeyaeleza. Leo tunataka tutangaze tena waombe, baadaye wajitoe, kisha tuwabembeleze, muda unakwenda tu! Hapana. Tuitendee haki nchi yetu,” amesema waziri mwandamizi.

Kuna taarifa kuwa kampuni nyingi za China zinajitoa katika mchakato mara zote ili kulinda masilahi yao nchini Kenya. 

Wakati wanajenga reli ya kutoka Mombasa hadi Nairobi, walilenga reli hiyo iende hadi Uganda, Rwanda na Burundi, hivyo mpango wao wa biashara ulilenga wapate faida kwa njia hiyo. Kitendo cha Tanzania kuanza kujenga reli ya kisasa kinaelekea kuvuruga mpango wa biashara wa Kenya, hivyo kuifanya reli ya Tanzania kuwa na mzigo mwingi kuliko ya Kenya.

Ukiacha eneo la kijiografia la Tanzania, reli inayojengwa Tanzania ni ya umeme ikilinganishwa na ya Kenya inayotumia dizeli. Uwezo wa reli hii ya Tanzania kubeba mizigo ni ekseli ya tani 35 wakati Kenya ni ekseli ya tani 25. 

Kwa maana hiyo, reli ya SGR inayojengwa Tanzania ina uwezo wa kubeba mzigo mkubwa kuliko ya Kenya. Kwa kasi pia nako kuna tofauti. SGR ya Kenya inakwenda kilomita 80 kwa saa, wakati ya Tanzania inakwenda kilomita 160 kwa saa kwa treni za abiria.

JAMHURI linaendelea kufuatilia kwa karibu mchakato wa ujenzi wa SRG na litaendelea kuleta taarifa za kila hatua inayopigwa hadi ujenzi utakapokamilika.