*Mawaziri wakuu wastaafu wamtaka asitoe matamko

*Katibu Mkuu mstaafu CCM asema watampa somo vikaoni

*Profesa asema ni matokeo ya kuua Kivukoni, IDM na Monduli

*Jaji aonya matamko ni tanuri la migogoro, kutomheshimu Rais

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wiki moja baada ya Gazeti la JAMHURI kuchapisha taarifa za Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, kuvuka mipaka ya utendaji wake kikatiba, mambo makubwa yameibuka.

JAMHURI limepata fursa ya kuzungumza na mawaziri wakuu wastaafu watatu, Katibu Mkuu wa CCM (mstaafu), wanazuoni na Jaji (mstaafu), ambao wamemfunda Dk. Mpango aepuke mwelekeo wa kutoa matamko, kuwaambia mawaziri atawabana na kuelekeza watumishi wa umma kusimamishwa kazi.

“Hata sisi wastaafu tunapata tabu kidogo juu ya kinachoendelea. Inawezekana sasa tunayaona wazi madhara ya watu kutopita Chuo cha Siasa Kivukoni au IDM Mzumbe… ila kubwa sisi wastaafu tunayo nafasi ya kushauri na kupitia vikao vya chama tutatoa ushauri wetu kuepusha migogoro inayoweza kutokea kwa matamko anayotoa,” mmoja wa mawaziri wakuu waliopata fursa ya kufanya kazi katika Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili ameliambia JAMHURI.

Amesema uongozi unaendana na utamaduni wenye kuweka misingi ya kuepuka migongano. “Mimi nilidhani siku ile alipoapishwa akasema anatoa maelekezo kwa TRA wakusanye Sh trilioni 2 kwa mwezi na Rais akatengua kauli yake papo hapo kuwa ‘hataki kodi za damu’ angeelewa, ila ninaona anaendelea tu. Sasa huyu mwache tutamshauri ndani ya chama,” ameongeza.

Waziri Mkuu mstaafu mwingine amesema: “Mtafute Jaji [Joseph] Warioba au [Pius] Mzee Msekwa watakwambia. Mwalimu Nyerere aliyaona haya tangu mwaka 1984. Katika yale mabadiliko ya kwanza ya Katiba, aliwatuma wazee hao Ufaransa wakajifunze jinsi Waziri Mkuu na Rais wanavyokuwa na madaraka ya kiutendaji bila kugongana.

“Walipokuja hapa nchini, ndipo kikaingizwa kifungu cha kuwa Rais atashauriana na Waziri Mkuu katika kuunda Baraza la Mawaziri. Hili lilikuwa ni mahsusi kuhakikisha mawaziri watakapokuwa wanasimamiwa na waziri mkuu ambaye ni mtendaji mkuu wa shughuli za serikali ndani na nje ya Bunge, basi wajue kuwa waziri mkuu alishiriki kuwateua, hivyo kwa kiasi ana mamlaka nao,” amesema.

Juhudi za kuwapata Jaji Warioba na Mzee Msekwa hazikuzaa matunda baada ya kuambiwa Jaji Warioba yuko safarini na Mzee Msekwa yuko Ukerewe. Simu zao wote hazikupatikana pia.

Waziri Mkuu mstaafu mwingine, amesema alishangaa mno kuona Makamu wa Rais anaagiza mawaziri na kusema atawabana kweli kweli kule Mtwara: “Nilimwangalia kwenye TV Julai 26, 2002 na baadaye nikasoma Gazeti la Uhuru Toleo Na. 24072 la Jumanne Julai 27, 2021, nikabaki nimeshika mdomo. Hapana. Hana mamlaka hayo kwa mawaziri wala watendaji, isipokuwa kwa maelekezo ya Rais tu, na inabidi aliseme wazi hilo, kuwa ametumwa na Rais kusema hayo atakayoyasema.”

Wakati akizindua Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, Makamu wa Rais, Dk. Mpango, alitoa maagizo kwa wizara tatu: “Naibu Waziri wa Ardhi ninakuagiza ubaki hapa Mtwara, ninakuagiza uungane na Waziri wa (TAMISEMI), mkashughulikie migogoro ya ardhi iliyopo uwanja wa ndege na eneo la Magomeni, mfanye hivyo mniletee taarifa mimi mwenyewe,” linamkariri Gazeti la Uhuru.

Uhuru limemkariri akimwagiza pia Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kuhakikisha hadi kufikia Septemba, mwaka huu wananchi wa mkoa huo wawe wanapata maji safi na salama kwani ameshaweka jiwe la msingi la chujio la maji katika mkoa huo. Akamtaka na Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga, kumpa taarifa endapo tatizo la maji halitashughulikiwa ili amshughulikie waziri mhusika.

“Kulikuwa na malalamiko ya maji, nimeshakagua chujio la maji, ninakuagiza Mbunge wa Mtwara Mjini, kama wananchi hawatapata maji safi na salama, niambie nikusaidie, nimshughulikie Waziri wa Maji,” mwisho wa kumnukuu.

Waziri Mkuu mstaafu mwingine, ambaye naye kama wenzake alikataa asitajwe jina gazetini kwa maelezo kuwa wana nafasi ya kushauri ndani ya chama, amesema: “Niliposoma Gazeti letu la Uhuru, sikuamini. Nilijiuliza, Makamu wa Rais anawezaje kumshughulikia waziri? Sasa kama mawaziri wataamua kumjibu si anawachokoza?

“Yeye anachopaswa kufanya ni kusema, ‘nimeyasikia matatizo, nitayafikisha kwenye mamlaka ya uteuzi au nitawasiliana na mamlaka ya uteuzi kwa maelekezo.’ Lakini sasa hii ya kusema apelekewe ripoti mweyewe? Akiipata ataifanyia nini? Nadhani anahitaji kujifunza mipaka ya mamlaka ya kazi zake na aina ya matamko anayoweza kutoa… kama ni Mazingira na Muungano, huko hautasikia tukimshangaa.”  

Alipoulizwa iwapo utaratibu anaotumia Dk. Mpango anaona uko sawa, alisema: “Kufuatana na Katiba, madaraka yako chini ya Rais, na yeye anaweza ku-delegate (kukasimu) maana anapounda Baraza la Mawaziri ana-delegate. Katiba inasema Waziri Mkuu ndiye anayesimamia utendaji wa day to day (siku hadi siku), Waziri Mkuu yeye ana madaraka throughout the government (kwa serikali yote)… lakini Makamu wa Rais hana mamlaka ama ya kusimamisha au kufanya nini. Hana madaraka hayo.

“Political appointees (wateule wa kisiasa) aliye na madaraka juu yao ni Rais. Hakuna mtu mwingine. Lakini siku hizi unasikia waziri amshughulikie huyu, kama kuna mambo mengine kuna procedure (taratibu) zake, lakini wengi wanavyofanya sasa hivi si utawala bora.

“Kama ni civil servant (watumishi wa umma), kuna sheria. Mtu anaamuru kamata fulani, mimi ninaangalia ninashangaa maana hawana madaraka hayo. Kama mtu amekosea, basi wafuate taratibu za kisheria na si kila mtu kuonyesha ana mamlaka.

“Wengi wanafanya makosa hayo. Kama kuna mtu anayehusika ni Wizara ya Utumishi ndiyo inayohusika, lakini sasa ni kama hatufuati utaratibu, tunaiendesha nchi kwa matamko,” amesema na kuongeza:

“Kama akisema kwa mawaziri anakuwa anachukua powers (madaraka) ya Rais, unless (labda) awe amemruhusu, lakini hii ya kujiamulia tu, italeta mgongano mbele ya safari. Aiache Dk. Mpango, yeye ni msaidizi mkuu wa Rais Samia, alikubali hilo na ndio ukweli usiopingika.

“Kwa upande mwingine, anachofanya Dk. Mpango, Waziri Mkuu ni kama madaraka yake yamechukuliwa hivi. Wakurugenzi wa halmashauri wote wale kwa utendaji wanaripoti kwa Waziri Mkuu. Sasa Makamu wa Rais anapoagiza mkurugenzi wa halmashauri asimamishwe, hilo si eneo lake,” amesema.

Amesema wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, ilifika mahala Rais Nyerere akaunda Kamati ya Baraza la Mawaziri aliyoiita Crisis Committee of the Cabinet (Kamati ya Dharura ya Baraza la Mawaziri).

“Kamati hii ilikuwa inashughulikia – Uchumi, Ulinzi na Usalama, kwa mambo ya utendaji Rais akasema muwe mnakutana kama kuna jambo msisubiri cabinet, tekelezeni bila kusubiri mkiamua, ila kwa kujua yapo ndani ya mamlaka yake, ilikuwa tunamwarifu anasema ‘endeleeni.’

“Utaona hata katika mazingira kama hayo ambayo ameunda kamati na kuipa nguvu, bado ilikuwa tunarudi kwa Rais kupata maoni yake. Hii ina maana tunapotekeleza ilikuwa ni uamuzi kutoka kwa Rais mwenyewe. Hii tuliifanya hivyo kuepusha muda mrefu sana, lakini tunawasiliana naye ajue kila kinachoendelea ili kuepusha mgongano. Waziri si mteule wa Makamu wa Rais, hivyo hawezi kusema atamshughulikia.

“Bahati mbaya huyu Makamu hakupitia katika mkondo wa siasa. Alikuwa ni mtaalamu. Pili, ameingia serikalini karibu leadership (uongozi) mzima ni leadership ambayo imejichukulia madaraka, hauangalii kama kuna Katiba au sheria, kwa hiyo anahamisha mazoea ya Awamu ya Tano kwenda Awamu ya Sita, ambapo kila kiongozi alitaka kutisha watu kwa kujiita Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama badala ya nafasi yake halisi.”

Kuhusu utendaji wa mawaziri, Waziri Mkuu mstaafu, amesema anafurahi hawakai ofisini, ila wakati huo huo wanapaswa kukaa ofisini wakatengeneza utaratibu wa kupata mrejesho kutoka kwa watendaji kila sehemu nchini, badala ya kila wakati kuwa “kwenye field, kwani hakuna uwezekano wa kuwa kila mahala kwa wakati mmoja, nchi hii ni kubwa.”

Waziri Mkuu huyo anaeleza mshangao wake: “Kwa mfano kila mwanzo wa mwaka inatolewa deadline (makataa) ya kumaliza madarasa na madawati. Mawaziri wanashinda wanakimbizana, unajiuliza hili litaisha lini? Ungefanywa utafiti wa kujua madawati yanahitajika mangapi nchi nzima, walimu unao wangapi?”

Amesema mamlaka ya nchi yaliyopo kwa Rais, anaweza kukasimu sehemu yake kwa Makamu wa Rais au mtu mwingine kwa maandishi yenye maelekezo mahsusi. “Rais Nyerere, alikuwa anakwenda kupumzika Butiama mwisho wa mwaka, anaacha mamlaka kwa makamu wake. Kwa mfano, fuatilia [Rashid] Kawawa ndiye alimwapisha Jaji Warioba kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mwalimu alimteua Jaji Warioba Desemba 1975, Januari 1976 Kawawa akamwapisha kwa maelekezo mahususi ya maandishi.”

Amemtaka Makamu wa Rais ajue kwamba nafasi ya Waziri Mkuu ndiyo yenye nguvu: “Tusipoangalia kunaweza kuwapo conflict (mgogoro) kati ya Waziri Mkuu na Makamu wa Rais. Unaweza kutoa maagizo ya utendaji yakawa na element ya policy (viashiria vya sera). Policy (sera) ni ya Rais. Enzi zetu ukiona jambo limeletwa mbele yako na ni zito, basi unasema ninalipeleka kwa Rais, hulitolei kauli. Ukiona kuna shida unaweza kumshauri Rais.”

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Haji Semboja, ameliambia JAMHURI kuwa ubunifu uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa nia njema wa kufanya kazi nje ya taratibu za kisheria, huenda umeacha makovu na si wote watakaofanya uamuzi kwa nia njema.

“Serikali ya Awamu ya Tano ilifanya ubunifu ambao haupo kwenye Katiba au nini. Hata Marekani, walifanya vitu ambavyo havipo kwenye Katiba wakati wa uongozi wa Rais Trump. Kila mtu anafanya ni innovative leadership (uongozi wa ubunifu). Ili kuleta mabadiliko na maendeleo haraka inabidi mifumo ifanyiwe marekebisho, inawezekana tu iwapo yule kiongozi anachokifanya kinakuwa ni kwa masilahi ya nchi kwa sasa na baadaye.

“Kwamba analolifanya yuko genuine (halisi) hayuko corrupt (si mla rushwa), kama anafanya kwa masilahi mapana. Ndiyo maana baada ya JPM kuondoka watu wengi wakauliza Katiba ya zamani. Yeye [Magufuli] anaweza kuwa alikuwa not democratic (si mwanademokrasia), lakini genuine (halisi) kwenye development (maendeleo). Kuna vitu fulani alifanya Magufuli kiutaratibu vilikuwa nje ya sheria, lakini kwa sababu vilikuwa na nia njema tunamshukuru.

“Kwa mfano wafanyakazi hawakubadilishiwa mishahara, na mishahara siyo issue (suala) ya unapenda au haupendi, hakukuwapo na ajira mpya, ambazo ni strategic (za kimkakati), ajira lazima kwa maendeleo. Ukiangalia Katiba na sheria mbalimbali zinampa madaraka Rais,” amesema Prof. Semboja.

Ameongeza kuwa kuna hatari ya viogozi kutumia utaratibu wa serikali iliyopita bila kufuata miongozo au Katiba ya nchi, kumbe wanajisingizia kuwa wanafanya kwa mwelekeo wa hayati Magufuli, “lakini baadaye anazalisha matatizo.”

Amesema bado kuna kipindi cha mpito kutoka Awamu ya Tano kwenda Awamu ya Sita, ila kinachotakiwa ni kila mtu kufikiri vizuri na kuangalia Katiba, Sheria na Mipaka yake inaishia wapi. “Wana ‘hangover’ ya awamu ya Tano. Zamani ilikuwa mtu hawezi kuwa kiongozi, lazima apitie Kivukoni, IDM Mzumbe kusoma uongozi. Wengine Monduli kwa ajili ya ukakamavu… ilikuwa wanafundishwa nini unaweza kusema na nini hauwezi kusema. Vile ambavyo wanapaswa kuvisema waviseme,” amesema.

Ameongeza kuwa shida kubwa sasa hivi viongozi wengi wanakwenda sehemu hawajaandika chochote, “wanasema kutokea kichwani kama ni strategy (mikakati), sera, inapaswa kuwa iko katika maandishi, lakini kwa kuwa hawana, wanasema kila kinachowajia. Mwisho anajikuta anatoa tatizo mikononi mwake analipeleka kwa mwingine.

“Tusameheane, tuendelee kujifunza, ila mimi inaniumiza sana. Tuna nafasi ya kujifunza dunia inaishi leo na kesho, hawa wa sasa hivi waelimishwe wajue nafasi zao na kiwango cha madaraka yao,” amesema Prof. Semboja.

Mmoja wa makatibu wa CCM wastaafu, ameliambia JAMHURI kuwa nchi inaendeshwa kwa kutegemea mambo matatu: “Katiba ilivyo, namna inavyotekelezwa na imani ya watu juu ya Katiba yao, hivyo kama kuna mtu anaikiuka Katiba kwa kufanya kazi nje ya mipaka ya kikatiba basi arekebishwe na kujirudi.

“Mnaweza mkawa na Katiba nzuri sana, lakini utekelezaji wake ukaleta matatizo. Inategemea waendeshaji wenyewe ndio wenye Katiba yao, ndio wanaotoa miongozo, ndio wanaofanya uamuzi. Inategemea wanadamu.

“Hauwezi kumtengeneza binadamu aitwaye kiongozi, alivyoumbwa na Mungu ndiyo hivyo hivyo, unaweza kumsaidia kwa mafunzo, lakini binadamu ana miondoko yake ya kiutu na ubinadamu. Ukitambua hivyo, unaweza kulazimika kukubali yanayotokea na kwamba hayana dawa nyepesi.

“Kama miondoko hiyo haileti tabu unaiacha, ila kama tunaona inaleta shida mbele ya safari, sisi wastaafu tuna vikao vya kushauri walioko madarakani – Kamati ya Viongozi Wakuu Wastaafu kwenye Katiba ya Chama, hiyo ni kikao rasmi cha kuwashauri na kushauri viongozi walioko madarakani. Tutashauri kwenye vikao hayo unayoyauliza,” amesema.

Jaji wa Mahakama ya Rufaa mstaafu (jina linahifadhiwa) amesema: “Makamu wa Rais anapofikia hatua ya kuwaagiza mawaziri ambao hajawateua, huo tayari ni mgogoro. Maana wasipotekeleza atawafanya nini? Hii si ni kujiaibisha tu? Lakini anatafuta kujenga mgogoro na Rais. Maana akienda akamwambia mfukuze waziri fulani hakutekeleza agizo langu na Rais akakataa, basi wataishi kwa misuguano ya chini kwa chini.

“Kuepuka yote hayo, Makamu wa Rais anapaswa kuchukua Katiba akaisoma vizuri, na aangalie miongozo aliyopewa alivyoingia ofisini. Yeye ni mtu wa kusema nimeliona, nashauri, tumepokea, nitawasilisha kwa mamlaka ya uteuzi na mengine ya hivyo. Makamu hawezi kusema nitambana waziri. Kwa sheria ipi?”

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Ibara ya 47 (1), Makamu wa Rais ana majukumu yafuatayo kisheria: “47.-(1) Kutakuwa na Makamu wa Rais ambaye atakuwa ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano kwa jumla, na hususan- (a) atamsaidia Rais katika kufuatilia utekelezaji wa siku hata siku wa Mambo ya Muungano; (b) atafanya kazi zote atakazoagizwa na Rais; (c) atafanya kazi zote za Rais kama Rais hayuko kazini au yuko nje ya nchi.”

Wachambuzi walianza kupata wasiwasi kuwa Dk. Mkapago anavunja Katiba baada ya kumwagiza Naibu Waziri wa Wizara ya Tawala za Mikao na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Festo Dugange, kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Hamis Dambaya, kwa alichodai ni matumizi mabaya ya Sh bilioni 2.2 kujenga Stendi ya Wilaya ya Nanyubu wiki tatu zilizopita.

Hadi sasa JAMHURI halijafanikiwa kumpata Makamu wa Rais, Dk. Mpango, ila litaendelea kumtafuta kupata ufafanuzi juu ya utaratibu wake wa kutoa matamko, maagizo na sasa kuwasimamisha watumishi wa umma kinyume cha Katiba au mamlaka yake kisheria.

1915 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!