Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar ea Salaam

Wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group iliyopo TAZARA wilayani Temeke kwa huduma bora za matibabu inazozitoa kwa wagonjwa.

Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na wanachama wa mfuko huo waliofika katika hospitali ya JKCI Dar Group kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.

Mwalimu Gloria Mwakasege mkazi wa Ukonga Dar es Salaam ambaye alimpeleka mtoto wake kutibiwa katika hospitali hiyo alisema baada ya kusikia kuna baadhi ya hospitali hazipokei kadi za NHIF alipata hofu kama anaweza kupata huduma lakini baada ya kufika katika hospitali hiyo alipokelewa na kupata huduma ya matibabu.

Watoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group iliyopo TAZARA wilayani Temeke wakimuhudumia mgonjwa

“Nimekuja hapa hospitali ya JKCI Dar Group na mtoto wangu ambaye anaumwa, huduma niliyoipata ni nzuri kwani mtoto ametibiwa na daktari wa watoto na kupewa dawa za kutumia kupitia kadi yangu ya bima ya NHIF”.

“Ninaziomba hospitali ambazo zimesitisha kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF zikae chini na Serikali wazungumze na kufikia muafaka kwani kuacha kwao kutoa huduma tunaoumia ni sisi wananchi”.

“Tunapopata changamoto za kiafya hasa nyakati za usiku maeneo ambayo ni rahisi kukimbilia na kupata huduma ni hospitali binafsi ambazo nyingi ziko karibu na makazi ya wananchi”, alisema Mwalimu Gloria.

Naye Julius Mwanyonga mkazi wa Yombo Dar es Salaam aliyefika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma za matibabu alisema  kupitia kadi yake ya NHIF amepata matibabu na dawa na hajapata shida yoyote ile wakati wa kupata huduma.

“Ninawaomba wananchi wenzangu ambao watapata shida ya kadi zao kutokupokelewa katika hospitali zingine waje hapa JKCI Hospitali ya Dar Group wanapokea kadi za NHIF na watatibiwa”, alisema Mwanyonga.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi  wa JKCI Hospitali ya Dar Group Iddi Lemmah alisema wanawapokea wagonjwa wanaotumia kadi za bima mbalimbali ambazo wameingia nazo mkataba wakiwemo wa NHIF pia wanawapokea wagonjwa wasiokuwa na kadi za bima ya afya  ambao wanapata huduma zote za matibabu na dawa wanazotakiwa kupewa kutokana na magonjwa waliyonayo.

Lema alisema kutokana na mabadiliko yaliyofanyika katika vitita vya NHIF kuna baadhi ya hospitali zimekataa kuwatibu wanachama wa NHIF lakini wao wanawapokea na  kuwapa huduma.

“Katika hospitali hii tunatoa huduma za matibabu na vipimo  kwa saa 24 hivyo basi wananchi wanapopatwa na matatizo mbalimbali ya kiafya wasiogope wafike katika hospitali yetu kwa ajili ya kupata huduma”, alisema Lemmah.

Alizitaja huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo kuwa ni pamoja na matibabu ya moyo, kinywa na meno, huduma za dharura, kliniki ya wanawake na wajawazito, kliniki ya watoto, macho, pua, masikio na koo, kliniki ya ngozi, vibofu vya mkojo, upasuaji mkubwa na mdogo, magonjwa ya tumbo na ini, figo na matibabu mengine ya magonjwa yanayoambukiza kama malaria.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam pia inatoa huduma za matibabu ya moyo ya kibingwa kwa wagonjwa mbalimbali wakiwemo wanachama wa NHIF.

By Jamhuri