Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Tabora

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Burian ameungana na Mashehe wa Mkoa huo, waumini wa dini ya Kiislamu na mamia ya wakazi wa Mkoa huo kumwombea dua Rais Mstaafu wa awamu ya pili Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi (98) aliyefariki dunia juzi jijini Dar es Salaam.

Akiongea katika ibada hiyo maalumu iliyoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Balozi Dkt .Batilda ametoa salamu za pole kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi kwa kuondokewa na Kiongozi aliyetumikia taifa kwa mafanikio makubwa sana.

Amesema kuwa yeye binafsi na wakazi wote wa Mkoa huo watamkumbuka kwa mchango wake mkubwa wa kimaendeleo alioutoa kwa Mkoa huo na taifa kwa ujumla akiwa madarakani enzi za uhai wake.

‘Jana tumefungua kitabu cha maombolezo Kimkoa kwa ajili ya kumbukumbu ya Mzee wetu Hayati Rais Ali Hassan Mwinyi kutokana na mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya nchi hili na Mkoa wetu’, ameeleza.

Balozi Batilda ametaja baadhi ya alama zilizopo katika Mkoa huo ambazo ni kumbukumbu nzuri ya kazi yake kuwa ni uwepo wa shule za sekondari zilizopewa jina lake na uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu wa Ali Hassan Mwinyi.

Ameongeza sifa nyingine za kipekee alizokuwa nazo Hayati Mzee Mwinyi na kumfanya awe kipenzi cha watu wengi kuwa ni ucheshi, mtu asiyependa makuu, mcha Mungu, mpole, mnyenyekevu, asiyependa dhuluma na mpenda maendeleo.

Shehe wa Mkoa wa Tabora Alhaj Ibrahimu Mavumbi amesema kuwa maisha ya hayati Rais Ali Hassan Mwinyi yalikuwa hadithi nzuri na tamu miongoni mwa jamii kutokana na unyenyekevu wake mbele za Mwenyezi Mungu.

‘Kwa niaba ya Shehe Mkuu na Mufti wa Tanzania, tunatoa pole nyingi sana kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi kwa kuondokewa na Mzee wetu’, amesema.

Awali Shekhe wa Wilaya ya Tabora Shehe Ramadhan Rashid amesema kuwa wameandaa ibada hiyo ya kumwombea dua ili Mwenyezi Mungu amwondolee adhabu ya kaburi na amfufue siku ya mwisho.

Ameongeza kuwa wakazi wa Mkoa huo na taifa kwa ujumla wamepoteza Kiongozi aliyekuwa ndani ya mioyo yao kutokana na utumishi wake mzuri, unyenyekevu, subira na msamaha, hivyo akatoa wito kwa viongozi wengine kuiga mfano huo.

Naye Kada wa Chama Cha Mapinduzi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani hapa Said Ntahondi amesema kuwa atamkumbuka Mzee Mwinyi kwa kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini ikiwemo kuhamasisha jamii kufanya kazi kwa bidii, alifungua milango kwa wafanyabiashara kuagiza bidhaa kokote kule.

Amebainisha kuwa Hayati Mzee Mwinyi hakupenda uonevu kwa jamii anayoiongoza, alikuwa tayari kuwajibika mambo yalipoenda vibaya, alishawahi kumpa siku 3 Waziri wake ili wakulima wa tumbaku walipwe fedha zao.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Tabora Mohamed Abeid ametoa wito kwa jamii kuwapa malezi mema watoto wao ili kuenzi maisha mazuri ya Hayati Mzee Mwinyi.

By Jamhuri