Na Zulfa Mfinanga, Jamhuri Media,
Dar es Salaam

Wanaharakati wa jinsia wametakiwa kuhakikisha kuwa elimu ya Usawa wa Kijinsia pamoja na elimu ya haki sawa inatolewa kuanzia ngazi ya familia kwa kuwashirikisha watu wote bila kubagua ili kila mmoja ndani ya Jamii atambue umuhimu wa suala hilo.

Hayo yamezungumzwa leo wakati wa ufunguzi wa Tamasha la 15 la Jinsia ambalo linaenda sanjari na kusherehekea miaka 30 ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), jijini Dar es Salaam na Naibu wa Rais Mstaafu wa Afrika Kusini kwa kipindi Cha mwaka 2005-2008 Phumzile Mlambo Ngcuka ambaye alikuwa mgeni rasmi wa tamasha hilo.

Naibu wa Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Phumzile Mlambo Ngcuka

Ngcuka ambaye pia amewahi kuwa Mkurugenzi wa shirika la Kimataifa la UN-Women amesema mfumo dume siyo rafiki Kwa wanawake hivyo wanaume hawana budi kushirikishwa ili kuweka mahusiano mazuri Kati ya jinsi zote.

“Kabla ya mkutano wa Beijing madhila Kwa wanawake Tanzania yalikuwa hayana mfano, licha ya kuwa bado kuna safari ndefu ya ukombozi lakini mkutano ule umechochea mafanikio haya yote tunayozungumza leo yakiwemo elimu kwa mtoto wa kike, ulinzi Kwa mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni, ukeketaji pamoja na shughuli ngumu ndani ya familia” amesema Ngcuka na kuongeza.

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Lilian Liundi.

“Na harakati hizi zitazaa matunda iwapo tutakwenda sambamba na marika yote bila kujali Jinsia, umri, dini, ukabila wala rangi lakini pia nisisitize kuwa hakuna mwanaharakati mwenye sura ya kibaguzi, mchochezi au anayependezwa na kile kinachoendelea Palestina…… mwanaharakati wa ukombozi wa kweli anatakiwa kuona haya siyo sawa katika Jamii”

Aidha amewataka wanaharakati kushikamana na kunyanyuana na wala siyo kusukumana ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma Kwa kuwa dira ya usawa wa kijinsia ni kumuwezesha kila mtu ili ifike hatua ya wanaume kuwa mstari wa mbele kutetea usawa wa kijinsia na kupinga mfumo dume ndani ya Jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Lilian Liundi amesema mada kuu ya Tamasha hilo ni miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi Kwa wanawake ambapo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996 zaidi ya watu 35,000 wamefanikiwa kuhudhuria na kupata kusikiliza sauti za pamoja na kujua mafanikio, mikakati na changamoto za Mtandao huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Gemma Akilimali amesema tafiti pamoja na mijadala mbalimbali iliyofanywa imesaidia kuleta mabadiliko ikiwemo kuanzishwa Kwa shule za awali pamoja na vituo vya kulelea watoto wadogo lengo ni kumpunguzia mwanamke majukumu ili kupata kupata muda wa kujiongeza kiuchumi.

“Pia serikali kutoa mwongozo wa Kila sekta kutengeneza bajeti yenye mrengo wa kijinsia pamoja na kuangalia ni kundi gani linahitaji bajeti zaidi ni miongoni mwa mafanikio yaliyoletwa na Mtandao huu” alisema Akilimali.

Shirika la Tusonge la mjini Moshi ni miongoni mwa wadau waliohudhuria Tamasha hilo ambapo hivi sasa shirika hilo linatekeleza mradi wa kukuza usawa wa kijinsia kwa kutumia mkabala wa haki za binadamu kwa makundi ya wanawake, watu wenye ulemavu na watoto katika Kata ya Bomambuzi iliyopo wilaya ya Moshi, Kata ya Biriri iliyopo wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro pamoja na Kata ya Maruvango iliyopo wilaya ya Meru na Kata ya Sokoni 1 iliyopo wilaya ya Arusha katika mkoa wa Arusha.

Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Gemma Akilimali.

By Jamhuri