Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Mbinga

WANANCHI wa vijiji vya Likwela na Unyoni vilivyopo kata ya Unyoni Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wameipongeza serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea miundombinu ya umeme ambapo toka uhuru hawajawahi kupata huduma hiyo.

Pongezi hizo wamezitoa leo kwenye mkutano uliofanywa na shirika la umeme Tanzania (Tanesco)mkoani Ruvuma ikiwa na muendelezo wa ziara ya afisa uhusiano wa huduma kwa wateja wa shirika hilo Allan Njiro la kutoa Elimu kusikiliza kero na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu umeme.

Afisa uhusiano wa huduma kwa wateja Tanesco Mkoa wa Ruvuma Allan Njiro akizungumza na wananchi wa kata ya Unyoni kwenye ziara yake ya kutoa elimu, kusikiliza kero na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu umeme.

Bw. Ndinus Ndungunguru mkazi wa Kijiji cha Likwela amesema kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapelekea miundo mbinu ya umeme kwenye kata hiyo lakini kuna baadhi ya Vijiji ndani ya kata ya Unyoni havijafikiwa bado hivyo wanaiomba serikali kuharakisha ujenzi wa miundombinu hiyo kwa kuwa kukamilika kwake kutaharakisha maendeleo kwa wananchi ikiwemo ufunguzi wa viwanda vidogo,saloon pamoja na uuzaji wa vinywaji baridi.

” Tunashukuru sana kwa raisi wetu Dkt. Samia kutuletea umeme lakini tunamuomba atumalizie vijiji vilivyobaki kama kule Ndolela hatuna umeme na nguzo tunaziona hatujui tatizo nini lakini pia kwenye zile huduma za kijamii kama Zahanati na shule pia ni muhimu kutuwekea umeme”alisema Bw. Ndunguru.

Agnes Mahangula amelipongeza shirika la umeme Tanzania kitengo cha huduma kwa wateja(Tanesco) mkoani Ruvuma kwa kitendo cha kukaa na wananchi na kusikiliza kero zao kuhusiana na umeme jambo ambalo linawarahisishia wananchi kutembea umbali mrefu kwenda kupeleka changamoto zao Wilayani hivyo ameomba na mashirika na taasisi za serikali kuiga mfano huo kwani huko vijijini wananchi wengi wanachangamoto nyingi sana.

Naye Afisa uhusiano wa huduma kwa wateja Tanesco mkoani Ruvuma Allan Njiro amesema kuwa ziara yake hiyo ya kutoa Elimu, kusikiliza kero na kutatua changamoto kwa wananchi wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa na wateja wengi wamepatiwa majibu ya maswali yao ambayo walikuwa nayo kwa muda mrefu na kwamba Changamoto zingine wamezichukuwa wataenda kuzifanyia kazi.

Amesema kuwa wateja wengi wamefurahia kwa sababu Vijiji vingi vipo mbali na makao makuu ya Wilaya na inawalazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma huku nauli zikiwa bei kubwa.

Baadhi ya wananchi wa kata ya Unyoni wakimsikiliza afisa uhusiano wa huduma kwa wateja Tanesco mkoani Ruvuma

By Jamhuri