Wananchi wa Mugango-Kyabakari-Butiama kupata maji Juni mwaka huu.

Na Jovina Massano, Msoma.

Mradi wa maji ya Ziwa Victoria  ulioanzishwa na Hayati baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere mwaka 1974 kutokea Musoma vijijini kuelekea wilayani Butiama mkoani Mara wafikia asilimia 73 . 

Mara baada ya kukamilika kwa Mradi huo kipindi Cha Mwl. Nyerere na maji kufika nyumbani kwake wananchi wa vijiji ilikopita miundombinu hiyo walitoboa mabomba hayo na kuweza kujipatia maji na kusababisha maji kutofika tena wilayani Butiama kwa kuwa nao walikuwa wanakabiliwa na uhaba wa maji ndio ukawa mwanzo wa kuharibika kwa Mradi huo.

Serikali kupitia wizara ya maji waliamua kuanza kukijenga upya ambapo waliuongeza ukubwa ambapo utahudumia vijiji 39 inakopita miundombinu ya mabomba hivyo uharibifu wa awali hautaweza kutokea kwa kuwa wahitaji wa maeneo hayo watanufaika na Mradi huo.

January 14,2023 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,mifugo na Maji ilitembelea Mradi huo na kuridhishwa na kasi ya ujenzi unaotekelezwa na kampuni ya UNIK Construction Engineering Lesotho (Pty) Ltd na Msimamizi

Sajdi Consulting Engineering Centre ya Jordan ikishirikiana na G-PES Engineers ya Tanzania na kuwataka wananchi  kulinda mradi huo.

Akizumgumza na Waandishi wa Habari Makamu Mwenyekiti ambae amekaimu nafasi ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Almas Maige mbunge wa jimbo la Tabora Kaskazini (Uyui) amesema kuwa mkandarasi ametekeleza mradi kwa viwango na kwa thamani ya pesa iliyotolewa.

“Kazi ya kamati hii ni kuisimamia na kuishauri Serikali katika maendeleo ya wananchi tumekuja hapa kuwawakilisha,katika miradi hii mikubwa ya maji mikoa ya Mwanza na Mara lengo letu ni kupata picha halisi ya namna miradi inavyoenda,tumeridhishwa na mradi huu wa Mugango Kyabakari-Butiama kwa kuwa utekelezaji wake umeishafikia asilimia 73 nampongeza mkandarasi na wasimamizi wa mradi huu wameutendea haki umewabeba wananchi wa wilaya husika nawaasa  kuthamini na kuilinda miundombinu hiyo kusiwe na uharibifu”, alisema Almas.

Aidha Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi amesema kuwa Mradi unaenda kwa kasi inayoendana na muda halisi,utekelezaji wake ni wenye tija ya kukidhi mahitaji ya wananchi kwa kuwapa huduma bora za maji.

“Wizara ya Maji kulingana na dhima ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuhitaji kuona wakina mama wanatua ndoo kichwani kutokana na kasi tunayoenda nayo tumetekeleza adhma hiyo tunajipongeza sisi watendaji wa wizara na kuna eneo ambalo limetengwa kwa uendelevu wa baadae hata watumiaji wakiongezeka utaendelea kukidhi haja kwa wahitaji,”amesema Maryprisca.

Aliongeza  Mbunge wa viti maalum anaewakilisha wafanyakazi  Janejelly James Ntate kuwa kulingana na kasi hii ya mradi maji yatafika sehemu zote zilizotengwa katika mpango wake kwa wilaya husika zote.

Nae Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini ambae pia ni mjumbe wa kamati hiyo Profesa Sospeter Muhongo amesema mradi huu utaondoa adha ya maji kwa wananchi wa vijiji vya Musoma vijijini na Butiama.

Alifafanua kuwa Choteo la mradi huu limejengwa kijiji cha Kwibara Kata ya Mugango Musoma vijijini lina uwezo wa kuzalisha lita Million 35 kwa siku ambao utahudumia vijiji 39 linakopita bomba kubwa.

“Mradi huu mpaka kukamilika kwake utakuwa umeghalimu kiasi cha Tsh bilioni 70.5 za wafadhili kutoka Serikali ya Saudi Arabia 49.12%, BADEA 31.40%na za Serikali ya Tanzania 19.48% na unatarajiwa kukamilika June mwaka huu”,amesema Muhongo.

 Aliongeza  kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mpango wake wa kumtua mama ndoo kichwani kupitia wizara ya Maji imeongezwa  Tsh bilioni 4.775  kwa ajili ya  kujenga miundombinu ya usambazaji wa maji(matoleo) kwenye vijiji vilivyo pembezoni mwa bomba kubwa mita 12 kutoka bomba kuu zikiwemo na Kata 2 za Mugango na Tegeruka.

Mhandisi Mkazi Chrispin Mwashala ameieleza kamati hiyo kuwa Bomba limezama Ziwani mita 1 chini ya ziwa(lake bed) na linapeleka maji kwa muaanguko wa mseleleko hadi kwenye kituo cha kusukumia maji kutoka ziwani( Low Lift Pumping Station)ambapo bomba kutoka ziwani linafikia urefu wa mita 9 chini ya ardhi ndani ya ziwa mdomo wa kuchotea maji uko mita 3.5 chini ya usawa wa ziwa na Mita 1 juu. 

Aleendelea kusema kuwa bomba linaanzia mita 200 ndani ya ziwa na nchi kavu mita 70 lipo nchi kavu bomba lina kipenyo cha mita 1 na urefu wake ni jumla ya mita 270.

Aliongeza kuwa walifanya utafiti wa historia ya kupungua kwa kina cha maji walibaini kuwa eneo hilo maji huwa hayapungui sana kwa mujibu wa wenyeji wa eneo hilo linakojengwa chujio la maji hivyo hakutakuwa na athari za uzalishaji pia utafiti huo ulionyesha kuwa Mwaka 1964 na 2006 kina cha maji katika ziwa kilipungua lakini eneo hilo halikuathirika hivyo hakutakuwa na changamoto ya uhaba wa maji kwa wananchi.

Alimalizia mwenyekiti wa bodi ya maji Mugango-Kyabakari-Butiama Chifu Jafet Wanzagi kwa kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa jitihada za kuhakikisha wananchi watapata huduma bora za maji Safi na salama na kuahidi kuutunza kwa kushirikiana na wananchi