Na Suzy Butondo, Jamhuri Media Shinyanga

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dk. Luzila John amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yakichangia vifo vingi vya watu ambayo mara nyingi yamekuwa yakishambulia moyo, hivyo amewataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara, kwani magonjwa hayo hayana dalili yoyote.

Hayo ameyasema leo wakati akitoa mafunzo maalumu ya afya, biashara pamoja na kaya na familia, iliyoandaliwa na kanisa la Waadventista Wasabato jimbo la Shinyanga (NGBF) ambayo ilifanyika katika ukumbi wa mikutano katika hoteli ya Makindo manispaa ya Shinyanga, ambayo yatafanyika kwa muda wa siku saba

Dk. Luzila amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza huchangia vifo vya watu wengi, ambayo mara nyingi hushambulia moyo na visababishi vyake ni matumizi ya tumbaku, ulevi uliokithiri, kutofanya mazoezi, kutozingatia mlo kamili, na uchafuzi wa hali ya hewa.

Mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Shinyanga Jonathan Manyama akifundisha somo la biashara kwenye semina hiyo

Luzila amesema wagonjwa wa kisukari asilimia 76 wanakufa na ugonjwa wa moyo kwa sababu moyo ni kiungo cha kwanza kinaathiriwa na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa, ugonjwa wa kisukari unaweza kuathiri karibu kila kiungo katika mwili, ikiwa ni pamoja na Moyo, mishipa ya damu, Macho, Figo, mishipa, njia ya utumbo, ufizi na Meno.

“Niwaombe tu wananchi wote muwe mnapima mara kwa mara afya zenu na mtu ukifikisha miaka 18 unaanza kupima mara moja kwa mwaka, ili kuweza kuzuia magonjwa haya na kujua kama utakuwa na magonjwa unafanyiwa matibabu kabla ugonjwa haujakuwa mkubwa ikiwa ni pamoja na kuzuia ugonjwa ulionao usiendelee kusambaa mwilini,”amesema Luzila.

Mwenyekiti wa Chemba (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga Jonathan Manyama alipokuwa akifundisha somo la biashara amesema kati ya watu 100 watu 68 hawana kazi za kufanya na hawajui kesho yao inakuwaje, ukitoa wazee na watoto asilimia 14 ndiyo wanafanya biashara.

Mganga mfawidhi wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Luzila akifundisha kwenye semina hiyo

“Mwandishi Robart Kiyosaki anasema kundi la kwanza la watu walioajiliwa wapo katika hatari kubwa ya umasikini na watu wa kwanza kuathirika ni wale walioajiliwa yaani wanaitwa watumwa wa fedha, na kundi la pili ni la watu waliojiajili yaani kupata fedha mpaka atoke mwenyewe, hivyo akiugua hapati fedha,”ameeleza Manyama.

“Na kundi la tatu walioajili watu wapo kwenye kundi la uhuru wa kifedha na kundi la nne ni la wawekezaji wapo katika uhuru wa fedha, akipata tatizo la aina yoyote au ugonjwa wowote hana wasiwasi fedha atakuwa nayo, hivyo ni vizuri wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali za kibiashara kwani fedha zimejificha kwenye mikono ya watu”ameongeza Manyama.

Kwa upande wake Mchungaji Mstaafu Wilbert Nfumbusa, akifundisha somo la Kaya na Familia, ametaja siri kubwa 4 za kufanya Familia kuwa na Furaha, ambapo ni kujipenda wewe mwenyewe, kumpenda jirani yako ambaye ndiye mwenzi wako kama nafsi yako ya pili, kumpenda Mwanao kama sehemu ya yako mwenyewe,pamoja na kumpenda Mungu kuliko vitu vyote.

Mwenyekiti wa mafunzo hayo Dk. Ellyson Maeja akizungumza kwenye semina hiyo

Naye Mwenyekiti wa Semina hiyo Dk. Hellyson Maeja, amesema lengo lake ni kukutanisha watu mbalimbali, kufahamiana pamoja na kupata Mafundisho kutoka kwa wataalamu wa Afya, Wabobezi wa Biashara pamoja na Masomo ya Kaya na Familia.

Maeja amesema kwa upande wa wataalamu wa Afya watakuwepo Madaktari Bingwa akiwamo Dk.Luzila, ambapo Somo la Biashara litakuwa likitolewa na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Shinyanga (TCCIA) Jonathani Manyama, huku Somo la Kaya na Familia litatolewa na Mchungaji Mstaafu Wilbert Nfumbusa.

“Tunawakaribisha wakazi wote wa Mkoa wa Shinyanga mhudhurie kwenye Semina hii ambayo ni muhimu sana katika maisha yenu ya kila siku ili mpate kujifunza masomo mbalimbali na kubadili mwenendo wa maisha yenu kwani tumeanza leo na tutahitimisha tarehe 27,4, 2024 ,”amesema Dk.Maeja.

Mchungaji Mstaafu Wilbert Nfumbusa, akifundisha somo la kaya na familia, kwenye mafunzo hayo.

By Jamhuri