Wananchi wazuia msafara wa Waziri wa Maji

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Arusha

Waziri wa Maji Jumaa Aweso (kulia) akiwasikiliza Wananchi wa Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani Arusha ambao waliusimamisha msafara wake jana wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi wakilalamia kukosa maji.

Wananchi wa Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani Arusha wamezuia msafara wa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kulalamikia kukosa maji ya matumizi mbalimbali kwa muda mrefu.

Kufuatia hali hiyo Waziri Aweso amelazimika kuchukua maamuzi magumu ya kutangaza kuzivunja Jumuiya za Watumia Maji wa eneo hilo kwa kushindwa kutekeleza majuku vizuri.

Wananchi wakiwa na ndoo za maji na matawi ya miti wakati walipozuia msafara wa Waziri wa Maji Jumaa Aweso.

Amechukua uamuzi huo baada ya wananchi kuzuia msafara wake wakiwa na ndoo za maji,mabango na matawi ya miti wakitaka serikali ichukue hatua ya kutatua changamoto hiyo.

Wananchi hao wamemweleza waziri kuwa kumekuwa na upendeleo wa ugawaji wa maji machache yanayopatikana kwa kuwagaiwia wafanyabiashara wenye hoteli (camp) huku wananchi wakitaabika bila maji.

Wamesema Kamati za Maji ndio zimekuwa zikifanya kazi ya kupeleka maji kwa wafanyabiashara huku taasisi zikiwano shule zikinyimwa maji na kusababisha wanafunzi kushindwa hata kwenda kwenye vyoo.

Devota Martin mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Kigongoni amesema changamoto ya maji katika eneo la MtowaMbu linatokana na miundombinu ya maji kuwa midogo ambayo ilijengwa tangu mwaka 1970.

“Maji yanapelekwa kwa wenye fedha shule yetu Kigongoni hawaendi choo na hawapikiwi chakula kwasababu hakuna maji,” amesema.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akijibu malalamiko ya wananchi hao amesema serikali iliagiza Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wayaanishe maeneo yote yenye changamoto.

Kufuatia hali hiyo alimwita Meneja wa RUWASA Mkoa wa Arusha,Joseph Makaidi atowe maelezo kwa wananchi juu ya hatua zilizofikiwa mpaka sasa dhidi ya changamoto ya maji eneo la Mtowambu.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Arusha,Makaidi amesema zaidi ya Sh.bilioni 1.7 zimetengwa kwa ajili ya kumaliza tatizo sugu la maji katika eneo la Mtowambu.

Amesema kinachosubiriwa kwa sasa ni kukamilisha taratibu za manunuzi na hatimaye aweze kutangazwa mzabuni atajayeanza kujenga mradi wa maji.

Waziri wa Maji,Aweso amesema serikali iliwagiza RUWASA kuainisha maeneo yote yenye changamoto ya maji ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.

Katika hatua nyingine Waziri Aweso amelazimika kutembea kwa miguu na wananchi hao kwenda kwenye eneo ambalo wananchi hao walimweleza imefungwa barabara yakwenda zilipo oofisiya Jumuiya ya watumia maji wa eneo hilo kwa kujenga nyumba jambo ambalo limesababishana usumbufu.

Baada ya kufika katika eneo hilo na kujionea hali halisi Aweso alipimpigia simu Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa ambaye alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Monduli Frank Mwaisumbe ambaye alikuwepo eneo hilo kulishughulikia jambo hilo kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha.