Magreth Kinabo na Stanslaus Makendi, Dodoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Mustapher Siyani amesema kwamba uongozi wa Mahakama ya Tanzania utachukua hatua ya kumwajibisha mtumishi yoyote yule ambaye atakuwa ni kikwazo wa mabadiliko yanayofanywa na mhimili huo katika kuelekea safari ya Mahakama Mtandao ifikapo mwaka 2025.

Aidha, Jaji Kiongozi amewataka Watendaji wa Mahakama mbalimbali kutosita kuwachukulia hatua watumishi wazembe waliochini yao.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.

Siyani alizungumza hayo leo tarehe 3 Machi, 2023 wakati akifunga kikao kazi cha mapitio ya bajeti ya nusu ya mwaka 2022/23 na uchambuzi wa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2023/24 ya Mahakama kilichofanyika Jijini Dodoma, ambapo alisitiza ushirikiano wa utendaji kazi kwa watumishi hao.

‘‘Hakuna mabadiliko yanaweza kutokea bila uwajibikaji. Kila mmoja wenu ni lazima atimize wajibu wake kwa vitendo ili kuhakikisha anatimiza jukumu muhimu la suala la utoaji haki iliyo bora kwa usawa na wakati na kuendana na mabadiliko hayo,’’amesema Jaji Kiongozi.

Aidha Jaji Siyani amewataka kushirikiana katika utendaji kazi na kila mmoja kujiuliza kuwa anaisadiaje Mahakama ya Tanzania katika kusonga mbele na kupata mafanikio na kuondoa fikra kila kitu kitafanywa na Makao Makuu.

‘‘Kila mtu awajibike kwa nafasi yake mnapopanga bajeti vipaumbele viwe ni vya taasisi.’’ amesisitiza.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akitoa hotuba yake  leo   tarehe 3 Machi, 2023 wakati akifunga kikao kazi cha mapitio ya bajeti ya nusu ya mwaka 2022/23 na uchambuzi wa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2023/24  cha Mahakama ya Tanzania kilichofanyika Jijini Dodoma.

Aliwataka Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama mbalimbali kushirikiana katika kufanikisha mabadiliko hayo. Mafanikio yatapatikana kutokana na nafasi ya kila mmoja,’’ alisisitiza.

Siyani aliongeza kuwa huu ni mwaka wa kufanya mabadiliko ya kutoa huduma bora, hivyo kila mtu awajibike kwa hilo. Alisisitiza kuwa watumishi hao wanatakiwa kuwa wabunifu na kuwa na umiliki wa mabadiliko hayo. Pia wanapaswa kufahamu utamaduni wa Mahakama.

Kwa upande mwingine, Jaji Kiongozi aliwasisitiza wajumbe wa kikao kazi hicho, kuangalia vyema namna wanavyopanga bajeti za maeneo yao na kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kuzisaidia Mahakama za Mwanzo kwa kuwa asilimia 70 ya mashauri yanatoka katika Mahakama hizo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Viongozi wa Menejimenti ya Mahakama, Naibu Wasajili, Watendaji wa Mahakama, Mahakimu Wakazi Wafawidhi na Maafisa Bajeti kutoka Mahakama mbambali nchini.Caption.

Wajumbe wa kikao hicho wakimsikiliza Jaji Kiongozi.

By Jamhuri