Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Bodi ya Sukari Tanzania imewataka wafanyabiashara wanaouza na bei ya sukari isiyo halali kuacha mara moja na kwamba hatua kali za kisheria dhidi yao.

Agizo hilo limetolewa leo Januari 18, 2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Profesa Kenethy Bengesi , ambapo wamebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara ambao siyo waaminifu wanaouza sukari kwa bei isiyo halali wakati wananunua kwa bei ya kawaida hivyo na kuwafanya Watanzania kuishi kushindwa kumudu gharama za bidhaa hiyo muhimu.

” Bodi inatambua kuwa kila mkoa unatofautiana bei ya sukari hivyo wafanyabiashara wanaopandisha bei kwa maslahi yao binafsi tofafauti na bei halali ya mkoa huo tukiwabaini hatutawaacha tutahakikisha tuwachukulia hatua kali za kisheria kwani hatupendi kuona wananchi wakilalamika juu ya bidhaa hii muhimu kupandishiwa bei holela” amesisitiza mkurugenzi.

Akizungungumzia uhaba wa sukari uliopo kwa sasa Profesa Bengesi amesema haliyo imetokana na kunyesha mvua za El nino zilizoanza Oktoba 2023 na kupelekea mashamba ya miwa kujaaa maji pamoja na miundombinu ya barabara kuharibika hivyo kushindwa kuvuna miwa iliyotakiwa kupelekwa kiwandani kuchakatwa sukari .

” Mwaka huu tumezalisha tani 345,000 pekee ambazo hazitoshelezi lakini kawaida mahitaji huwa ni tani 520,000 na katika uzalishaji tunapenda malengo yetu ni kuzalisha tani laki tano na hamsini na tano ili tuwe na akiba ya sukari ya kutosha lakini kutokana Msimu huu wa mvua za El nino tumeshindwa kufikia lengo ndiyo maaana tuna uhaba wa sukari” amesema Bengesi.

Hata hivyo amebainisha Serikali imechukua hatua za kukabiliana na uhaba wa sukari kwa kutoa kibali kwa kuagiza sukari nje ya nchi tani 50,0000 na kwama sukari hiyo inatarajiwa kuingia nchini Januari 22 , 2024 .