Na Daniel Limbe, JamhuriMedia,Biharamulo

MATUMIZI mabaya ya dawa za kutibu ugonjwa wa shinikizo la damu(Viagra) unatishia ongezeko la vifo vya wanaume wilayani Biharamulo mkoani Kagera kutokana na baadhi ya watu kuzitumia holela kwa imani za kuongeza nguvu za kuhimili tendo la ndoa.

Imedaiwa kuwa dawa hizo zinauzwa holela kwenye maduka ya dawa muhimu za binadamu huku wanunuzi wakichukua pasipo kupata ushauri wa Daktari.

Mganga mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Dkt. Godfrey Masuki, amesema hayo wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo,na kuwasisitiza kusaidia kuelimisha jamii kubadili mfumo wa maisha kwa kujikita zaidi katika ulaji wa vyakula vya asili.

“Lipo tatizo kubwa la wanaume kutumia dawa za Viagra kuongeza nguvu za kiume,dawa hizo ni hatari unapozitumia pasipo maelekezo ya daktari ndiyo maana siku hizi vifo vya kushitukiza vya wanaume watu wazima kufia gesti vimekuwa vikiongezeka”amesema

“Dawa hizo ni maalumu kwaajili ya kutibu magonjwa ya moyo lakini watu wanazitumia kusisimua misuli kwa lengo la kuongeza nguvu za kiume jambo ambalo ni hatari zaidi kwa afya zao” amesema Dkt. Masuki.

Ofisa lishe wa wilaya hiyo,Domina Jeremia,amesema suluhisho la upungufu wa nguvu za kiume ni watu kurejea kwenye ulaji wa vyakula vya asili ili kuongeza vitamini mwilini badala ya kuhangaika na matumizi ya vyakula vingi vya viwandani.

“Tunawashauri wananchi watumie zaidi vyakula vya asili hasa vyenye asili ya mikunde,wapunguze sana ulaji wa wanga kwani inapozidi mwilini hugeuzwa kuwa sukari na kusababisha baadhi ya wananchi kukumbwa na Ugonjwa wa kisukari”.

“Tunapendekeza wanaume kutumia zaidi mbegu za maboga,maboga menyewe,
majani ya maboga na matunda kwa wingi,hii itawasaidia sana kurejesha nguvu zao za kiume badala ya kutumia Viagra”amesema Domina.

Hata hivyo elimu hiyo imeonekana kuwakuna sana madiwani hao na kusisitiza iwe endelevu hadi kwenye vijiji na kata hali itakayosaidia kupunguza uhasama kwa wananchi ambao hukimbilia kwa waganga wa Jadi kupiga ramli baada ya kutokea vifo vya ghafla.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu, amelazimika kutoa maagizo kwa idara ya afya kufanya operesheni maalumu ili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wamiliki wa maduka ya dawa za binadamu wanaouza Viagra kama njugu pasipo kuwepo kwa ushauri wa kidaktari.

                   
Please follow and like us:
Pin Share