Wanaume wawili ambao ni wakazi wa Kijiji cha Mkangaula , Kata ya Namalenga wilayani Masasi mkoani Mtwara wameuana kwa kupigana kwa kutumia magongo kwa kugombea mwanamke ambaye kila mmoja alidai ni mpenzi wake.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicomedus Katembo, amesema kuwa, marehemu hao Mussa Bakari (21) na Ibrahim Shabani (28), wote wakazi wa Kijiji cha Mkangaula mkoani Mtwara,wameuana baada ya kupigana kwa kutumia magongo wakigombea mwanamke aliyetambulika kwa jina la Hadija Msamati.

Kamanda Katembo amesema kuwa tukio hilo,lilitokea mwishoni mwa wiki, majira ya saa 12 jioni, katika Kijuji cha Mkangaula wilayani Masasi mkoani hapo.

“Ni kweli wanaume wawili wamekufa baada ya kupigana kwa sababu ya kugombea mwanamke ambaye kila mmoja alidai kuwa ni mpenzi wake,” amesema kamanda.

Kamanda Katembo amesema kuwa vijana hao waliuana baada ya kufumaniana na ndipo walipoanzisha ugomvi huo kwa kupigana kwa kutumia magongo ambapo kila mmoja alifanikiwa kumpiga mwenzake hadi walipofika hatua ya wote kuanguka chini na baadaye kupoteza maisha.

Amesema kuwa Jeshi la Polisi tunamtafuta mwanamke huyo kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Kamanda Katembo amesema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa jamii kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkoani badala yake wafuate kanuni na sheria ili kuepuka mambo ambayo yanaweza kujitokeza kama hayo ya mauaji.