Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Mtwara

Mkazi wa Kijijii cha Namanjele mkoani Mtwara,Somoe Mohamed anatuhumiwa kumchoma moto mtoto wake wa umri wa miaka mitano kwa madai ya kudokoa mboga.

Kwa mujibu wa majirani (jina linahifadhiwa),amesema kuwa wakati akiendelea kufua nyumbani kwake alisikia kilio cha mtoto wa jirani yake kwa muda mrefu na alipoamua kwenda alikuta mama yake akiendelea kumchapa huku mtoto akiungua.

“Hiki kitendo sikuweza kuvumilia niliamua kwenda kumuita jirani yangu ambaye alifika eneo la tukio na kisha tulifanikiwa kumuokoa huyo mtoto hata hivyo tuliamua kumpigia simu baba yake ambaye hakuwepo wakati wa tukio,” amesema.

Hata hivyo mama wa mtoto huyo amesema kuwa chanzo cha kumchoma moto mikono mtoto wake ni baada ya kudokoa mboga na pia kuiba sh.250 lakini nia yake ilikuwa ni kumuonya ili asiendelee na tabia hiyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa majirani ambaye hakupenda jina lake kuandikwa amesema kuwa hadi leo mtoto ana siku ya tatu tangu kuchomwa moto na hajapelekwa hospitalini.

Naye baba wa mtoto huyo,Juma Lubega amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa siku ya tukio hakuwepo lakini alipofika nyumbani na kumuona mtoto wake ameungua mikono na vodole alisikitika sana.

“Mimi kama baba wa mtoto nilisikia uchungu sana baada ya kumuuliza mke wangu akasema kuwa alifanya hivyo baada ya mtoto kudokoa mboga na kuiba sh.250 hivyo alimfunga kamba mikononi akaweka nyasi akamchoma mtoto,” amesema Lubega.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mussa Mkadimba amesema kuwa tukio hilo sio zuri kwa kuwa halifundishi mtoto bali linaweza kumfanya akawa katili.

By Jamhuri