Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waombaji wa mikopo ya elimu ya juu ambao wana taarifa za ziada ambazo hawakuziwasilisha katika maombi ya awali, wameshauriwa kuzitumia vyema siku saba kukata rufaa ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.

Wito huo umetolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ambapo rufaa hizo zinapokelewa kuanzia Oktoba 25 hadi 31, 2026.

Rufaa hizo ni mahsusi kwa waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2026/2027 huku lengo likiwa ni kuwapa waombaji hao nafasi ya kuwasilisha taarifa za ziada ili waweze kuzingatiwa katika utoaji wa mikopo hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, amesisitiza umuhimu wa kuzitumia vizuri siku hizo ili kuondoa malalamiko kwa waombaji wenye taarifa zinazoweza kusaidia kupangiwa mikopo kwa viwango wanavyostahili.

“Serikali kupitia Bodi ya Mikopo imedhamiria kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye sifa ya kupata mkopo anapangiwa mkopo … hivyo, siku saba za rufaa zilizotolewa zitumike vizuri kwa waombaji wote wenye vielelezo vya ziada vinavyoweza kusaidia kupata mikopo ya elimu,” amesema Dk. Kiwia.

Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, HESLB inatarajia kutumia shilingi trilioni 1.06 kwa ajili ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wasiopungua 300,000.

Aidha, fedha hizo ni ongezeko la asilimia 15.6 ikilinganishwa na shilingi bilioni 916.7 zilizotolewa kwa mwaka wa masomo 2025/2026 zilizogharimia masomo ya wanafunzi 289,932.