DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Baada ya Katibu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania, Jimbo Kuu la Kusini, Mchungaji Dk. Rabson Nkoko, kusema hakuna mgogoro wowote wa fedha unaofukuta, washiriki wengine wameibuka na kumtaka ajitokeze tena hadharani kueleza ukweli wa tuhuma hizo na si kujibu porojo.

Washiriki wamesema wanazo taarifa kwamba Mchungaji Nkoko ameitisha kikao cha dharura cha Kamati Tendaji ya Unioni Misheni ya Kusini mwa Tanzania kitakachofanyika Aprili 14, mwaka huu kinyume cha miongozo.

Wamesema kwa mujibu wa miongozo, Unioni hiyo inapaswa kuwa na vikao viwili tu ambavyo ni katikati ya mwaka na mwishoni mwa mwaka. 

“Sasa kama Mchungaji Nkoko anasema kanisa liko salama, je, hiki kikao kinachokwenda kutumia fedha nyingi za washiriki kulipa wajumbe ni cha nini?

“Watuhumiwa hao wameamua kuitisha kikao cha dharura kwa wajumbe wa Kamati Kuu ya

Unioni, wajumbe waalikwa na mwanasheria wa kanisa. Wakati kikao cha kawaida cha Kamati Kuu ya Unioni kilipangwa kufanyika kati ya Mei 5 hadi 9, mwaka huu kisha Mei 11, mwaka huu ndiyo siku ya kikao,” wamesema.

Pia wamesema wajumbe watakaohudhuria kikao hicho wanatakiwa kuwasili Aprili 13, mwaka huu na kuondoka Aprili 15, mwaka huu.

“Kwa kawaida hakuna kikao chenye jina la Extraordinary Ex Com katika Kanisa la Wasabato, maana vikao vyake rasmi ni viwili tu kwa ngazi zote za kanisa kuanzia konferensi ndogo (local conference) hadi konferensi kuu (general conference),” amesema mmoja wao na kuongeza:

 “Ambavyo ni kikao cha katikati ya mwaka (mid-year) na cha mwisho wa mwaka (year-end meeting). Lakini kama kuna dharura yoyote wataitisha kikao cha dharura kiitwacho (available excom meeting).

 “Lakini kitu cha kushangaza kikao chenye jina lisilo la kawaida kimeitwa kwa dharura kabla ya Mei na wajumbe wametakiwa kuzipitia tena ratiba zao na kufanya marekebisho kwa ajili ya kikao hicho.”

Vilevile wamesema Mwenyekiti wa Kamati Kuu Tendaji ya Unioni hadi sasa hana uhalali wa kuitisha kikao chochote kwa sababu yeye pamoja na Katibu na Mhazini wake ndio wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha na matumizi mabaya ya ofisi.

Katika kikao hicho, wanadai kuna ajenda ya kubariki makosa waliyofanya na kumwandikia barua Msajili wa Jumuiya na kumwambia hawatambui na wanakusudia kumpeleka mahakamani asiwakague kwa sababu walifanya hivyo bila kushirikisha Kamati Kuu Tendaji ya Unioni.

 “Wanafanya mpango wa kukwepa ukaguzi kwa watuhumiwa wote na namna ya kuwawezesha waendelee kukaa madarakani hadi mwisho wa mwaka wakati wa uchaguzi.

 “Lakini wanayafaya yote haya huku fedha za washiriki ndizo zinateketea katika kulindana madarakani. Mambo ya kujiuliza ni kwamba wananufaika na nini kwa kuendelea kukaa madarakani wakati kuna tuhuma nzito hivyo? Kwa nini wanatumia nguvu kubwa kunyamazisha ukaguzi usifanyike?” amehoji.

Washiriki wengine wanena

Wakizungumza na Gazeti la JAMHURI mwishoni mwa wiki iliyopita, washiriki hao (majina tunayahifadhi) wamesema tuhuma zote zilizopelekwa na wenzao watano kwa Msajili wa Jumuiya zina ukweli.

 “Kwa taarifa tu ieleweke kwamba waliopeleka malalamiko ya tuhuma hizo kwa Msajili wa Jumuiya ni wenzetu watano, lakini nyuma yao tuko zaidi ya 300 na hao ni wale tunaofahamiana,” amesema mshiriki mwingine na kuongeza:

“Tunamtaka Mchungaji Nkoko ajitokeze hadharani atueleze tuhuma ya matumizi mabaya ya kiasi cha Sh milioni 480 zinazotokana na asilimia nane ya sadaka ya washiriki kwa vyombo vya habari ambavyo yeye ndiye Mwenyekiti wa Bodi.

“Sisi washiriki tunamtaka tena ajitokeze hadharani alieleze kanisa na umma kuhusu tuhuma ziliko Sh bilioni 5.8 za iliyokuwa Konferensi ya Mashariki mwa Tanzania (ETC) baada ya kuvunjwa na kuundwa Konferensi mbili mpya za Mashariki Kati (ECT) na Kusini Mashariki (SEC).

“Kwa sababu SEC na ECT hazikugawiwa hata shilingi moja, vilevile hata mali kama vile magari na mashamba nayo hayajulikani yaliko pia. Tunamtaka tena ajitokeze aliambie kanisa na umma kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa Sh 18,000,000 za Shule ya Msingi Kongowe Adventist ziko wapi, kwa kuwa ndizo zilizomfukuzisha Mchungaji Kheri Kuyenga baada ya kuzihoji.

“Pia tunamtaka tena ajitokeze hadharani awaambie washiriki na umma ziliko Sh 97,000,000 za Shule ya Msingi ya Kongowe Adventist zilizobainika kupotea chini ya kamati ya uchunguzi ya Dk. Daniel Sabai.”

 Wamemtaka Mchungaji Nkoko ajitokeze hadharani mbele ya washiriki na umma, awaambie ziko wapi Sh milioni 400 zilizokarabati makao makuu ya ECT chini ya kiwango na makandarasi wawili ambao ni Mwaipungu na Singo wanaodaiwa kupatikana bila ushindanishaji wa zabuni.

 Pia wamemshangaa Mchungaji Nkoko kujibu tuhuma hizo kwa kulihusisha kanisa lote la Tanzania nzima.

“Tuhuma zilizopo zinawahusu viongozi wa eneo la kikanisa la Unioni Misheni ya Kusini mwa Tanzania, tena wametajwa kwa majina lakini majibu yake yamelijumuisha kanisa lote la Tanzania, nini kinatafutwa hapa?

 “Huku si kuingilia mamlaka ya Union Konferensi ya Kaskazini? Inakuwaje tuhuma  za watu binafsi kuhusishwa na kanisa lote nchi nzima, hii ikoje? Halafu kwa nini yeye akatae kuwa tuhuma hizo si za kweli bila uchunguzi wowote kufanyika? Kwa vile wanadai si kweli, basi watulie wachunguzwe na majibu ya kama ni kweli au si kweli yatatoka,” amesema.

Kuhusu jibu la Mchungaji Nkoko kwamba washiriki hao watano hawaheshimu mamlaka ya Kanisa la Wasabato na taratibu zake, wamesema suala hilo lipo kinadharia tu lakini si kwa vitendo kama inavyodhaniwa.

 “Hayo ni maneno tu, na kwa muktadha wa tuhuma hizi na nafasi za watuhumiwa ni kanisa lipi au mchungaji yupi angeweza kukubali kuzijadili na kuzipitisha tuhuma hizi ziende ngazi ya juu wakati watuhumiwa hao ndio wakubwa wake wa kazi?” amehoji mshiriki mwingine na kuongeza:

 “Kwa taarifa tulizonazo ni kwamba washiriki wenzetu waliokwenda kwa Msajili wa Jumuiya wako katika msukosuko mkubwa baada ya wachungaji wa mitaa kuagizwa na watuhumiwa kwa kofia zao za uongozi wa kanisa wa juu kuwachukulia hatua za kuwafuta ushirika ili kuzima tuhuma hizo.

 “Kwa mfano Kanisa la Kibulugwa SDA, Mchungaji wa Mtaa, Christian Kivuyo, alipeleka ajenda ya kumfuta Nathanael Bhubuli ushirika wake lakini ajenda hiyo ilipingwa na wajumbe wa baraza la kanisa lakini akatumia mabavu na kuipeleka katika mashauri ya kanisa napo ikatupwa mbali.

 “Pia Kanisa la SDA Mwenge, Mchungaji wa Mtaa, Elitabu Kajiru, aliitisha baraza la kanisa liidhinishe ajenda ya kuwafuta ushirika walalamikaji John Augustine na Nehemia Matiku katika baraza la kanisa na ajenda ilipitishwa ili iende katika mashauri ya kanisa.”

Katika hatua nyingine, wamesema yapo madai ya uongozi kuwaita washiriki waliokwenda kulalamika kwa Msajili wa Jumuiya lakini hakuna kilichofanyika. 

“Baada ya mkutano mkuu maalumu wa kulifuta Kanisa la SDA Temeke uliofanyika Machi 11, 2020, uongozi wa Unioni Misheni ya Kusini mwa Tanzania uliwaita washiriki hao Machi 15, 2020 kutoka SEC peke yake.

 “Kikao kilichodumu kwa saa nane tu lakini washiriki hao waliishia kubezwa, kukejeliwa na kupuuzwa licha ya kuwasihi watuhumiwa wajiuzulu ili kuepusha hatua nyingine lakini waliendeleza dharau na kiburi,” amesema mshiriki mwingine aliyeonekana kuwa na hasira kali.

Pia wamesema washiriki hao wakaiandikia Divisheni (ECD) barua na nakala yake wakaipeleka Konferensi Kuu (GC) inayohusu tuhuma zilizojadiliwa katika kikao hicho cha saa nane lakini Mwenyekiti wa Divisheni ya Mashariki Kati mwa Afrika akawajibu kwamba hizo ni ‘hadithi chafu’.

Vilevile wamesema wanashangazwa na kitendo cha watuhumiwa wa ubadhirifu huo kutumia mimbari za makanisa kujisafisha na kuwatuhumu washiriki waliopeleka tuhuma hizo kwa Msajili wa Jumuiya.

“Kwa taarifa tulizonazo zenye ushahidi na tutautoa itakapohitajika ni kwamba watuhumiwa walishachukua hatua za kuwashitaki washiriki waliokwenda kwa Msajili wa Jumuiya,” amesema na kuongeza:

 “Tuhuma hizi ni za watu binafsi hivyo watuhumiwa wasizihusishe na kanisa na waepuke kutumia majukwa ya kanisa kama wanavyofanya kujisafisha kwa sababu kanisa ni washiriki. 

“Halafu washiriki wengine katika Unioni ya Kusini mwa Tanzania wanapotoshwa kuwa watuhumiwa hao wanafuata taratibu za kanisa pasipokwenda katika vyombo vya sheria tofauti na walalamikaji.”

Aidha, wamesema kwa taarifa walizonazo ni kwamba watuhumiwa hao wanafanya mpango kuzuia wasikaguliwe kwa kudaiwa kuzunguka katika taasisi za serikali, kwa viongozi serikalini na kutafuta washiriki wenye nyadhifa serikalini na walio nje ya nchi wanaoweza kuwasaidia wasichunguzwe.

 Wiki iliyopita Gazeti la JAMHURI liliripoti kuwa washiriki wa kanisa hilo wanawatuhumu baadhi ya viongozi wao kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo ubadhirifu wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka.

 Washiriki hao ambao wako watano; Nathanael Bhubuli, Maila Makambi, Nehemiah Matiku, John Augustine na Machibya Mayala, wakaziwasilisha tuhuma hizo kwa Msajili wa Jumuiya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kuomba uchunguzi maalumu ufanyike.

 Kupitia barua waliyoandika Agosti 30, 2021 kwenda kwa Msajili wa Jumuiya, washiriki hao wanasema kuanzia mwaka 2014 hadi sasa kanisa lao katika Jimbo Kuu la Kusini, Konferensi ya Mashariki Kati (ECT) na Konferensi ya Kusini Mashariki (SEC) limeshindwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi na kuonyesha mali zao na kusababisha kutoaminiana kati yao na viongozi kwa kuwa hawataki kuwasikiliza. 

Licha ya kufanya hivyo na kuomba uchunguzi huo uanze mara moja lakini wanasema kwa bahati mbaya vinara wa tuhuma hizo ambao ni viongozi wao katika Unioni ya Kusini (STUM) na katika konferensi za ECT na SEC bado wapo ofisini na wana taarifa zinazodai kwamba wameanza kuharibu ushahidi na wanashauri wakae pembeni.

“Tunashauri wakae pembeni na kupisha uchunguzi utakaokuwa huru na haki. Malalamiko yaliyowasilishwa tuna hakika ni ya kweli na bado ubadhirifu unaendelea kufanyika kwenye kanisa letu, hivyo si vema watuhumiwa kuendelea kukaa ofisini wakati uchunguzi unaendelea,” wanasema.

Viongozi wanaoshauri wakae pembeni ili kupisha uchunguzi huo ni kutoka Unioni ya Kusini mwa Tanzania ambao ni Mchungaji Mark Malekana (Mwenyekiti), Mchungaji Nkoko (Katibu Mkuu), Athanas Sigoma (Mhazini Mkuu), Mchungaji Christopher Ungani (Mkurugenzi wa Mawasiliano) na Reuben Mbonea (Mhasibu wa Vyombo vya Habari).

 Kutoka ECT ni Mchungaji Joseph Mngwabi (Mwenyekiti), Mchungaji Amos Lutebekela (Katibu Mkuu) na Enock Rabieth (Mhazini Mkuu) na kutoka SEC ni Mchungaji Steven Ngussa (Mwenyekiti), Mchungaji Wilfred Mafwimbo (Katibu Mkuu) na Yusufu Zege (aliyekuwa Mhazini Mkuu).

Katibu Mkuu Nkoko ametoa tangazo katika gazeti la kila siku (jina linahifadhiwa) wiki iliyopita akikanusha kuwapo ubadhirifu katika Kanisa la Waadiventista Wasabato, Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania na kuwataka washiriki watulie kwani hakuna tatizo kwa maelezo yake.

By Jamhuri