Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Watu watano wamefariki kwa ugonjwa ujulikanao kwa jina la Marburg mkoani Kagera huku watatu wakiendelea kupatiwa matibabu katika vituo maalum vilivyojengwa
Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema uchunguzi uliofanywa na maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii umethibitisha uwepo wa virusi hivyo na kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) ugonjwa huo uligundulika kwa mara ya kwanza nchini Ujerumani 196.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imefanikiwa kudhibiti kasi ya maambukizi mapya ya ugonjwa huo na kuwataka Wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kuwaondoa hofu.

Amesema ugonjwa huo huambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hususani kwa njia ya kugusa maji maji kama vile mate, mkojo, damu, machozi au kinyesi yanayotoka kwa mtu mwenye dalili hizo.

Amesema maambukizi yanaweza kutokea pia kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu iwapo mtu atakula au kugusa mizoga au wanyama walioambukizwa.

“Dalili za ugonjwa huo ni homa,kuumwa kichwa, maumivu ya misuli, kuishiwa nguvu, kutapika, kuhairisha na kutokuwa damu sehemu za wazi za mwili ugonjwa huu hauna tiba.

“Hadi kufikia Machi 21,mwaka huu, ikiwa ni siku tano tangu kuripotiwa kwa watu wenye dalili jumla ya watu nane wameripotiwa kuwa na ugonjwa huo na kati yao vifo ni vitano huku wagonjwa watatu wakiendelea na matibabu katika vituo maalum vilivyotengwa mkoani Kagera “amesema.

Hata hivyo Waziri Ummy amewatoa hofu wananchi kuwa hadi sasa Serikali imefanikiwa kudhibiti kasi ya maambukizi mapya ya ugonjwa huu.

“Nitumie fursa hii kuwashukuru Uongozi na watumishi wa afya hususani walio mstari wa mbele mkoani Kagera ambao wanaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwahudumia wagonjwa na kuhakikisha ugonjwa huu unadhibitiwa.

“Vilevile ninaishukuru Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuungana na timu ya Mkoa wa Kagera kukabiliana na ugonjwa huu kwa wakati.

“Pia ninatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kwa Serikali endapo kuna tetesi za mhisiwa au mtu mwenye dalili za ugonjwa huu. Aidha endapo kuna mtu yoyote mwenye dalili za ugonjwa huu afike kituo cha kutoa huduma za afya kwa ajili ya Uchunguzi na Matibabu.

“Pia ninatoa Wito kwa watumishi wa afya kote nchini kuzingatia miongozo na Taratibu za Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi (Infection Prevention and Control) wakati wote wa kutoa huduma kwa wananchi,” amesema.

Kwa Upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Tumaini Nagu alisema kati ya wagonjwa hao nane,wawili ni wahudumu wa afya huku sita wakiwa wametokea familia moja.

Amesema kuwa hadi sasa jumla ya watu 161 wapo kwenye uangalizi maalum.

By Jamhuri