Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika uwekezaji katika Sekta ya Madini ili kuupiga jeki uchumi wa taifa kwa kutengeneza ajira na walipa kodi wapya.

Hayo yamesemwa leo Mei 20, 2024 na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba ikiwa bado siku mbili kufanyika kwa Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ambalo litaanza rasmi kesho kutwa Mei 22, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Arusha International Conference Centre (AICC).

Mhandisi Samamba amesema kuwa, kuna fursa nyingi katika Sekta ya Madini kutokana na mazingira bora yanayowavutia wawekezaji hivyo kuwataka watanzania kuchangamkia fursa hizo.

“Watu wajitokeze kwa wingi siku ya jukwaa ili kubaini fursa zilizopo katika sekta hii ya madini na kuzichangamkia,”amesema Mhandisi Samamba.

Aidha, amesema kuwa jukwaa hilo ambalo mgeni rasmi ni Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, litatoa elimu ya kuyafahamu mengi kutoka kwenye Sekta ya Madini na namna ya kuzifikia fursa zilizopo ili kuchochea zaidi ukuaji na mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa.

” Sisi tutahakikisha watanzania wanabaini na kuzichangamkia fursa zilizopo, kuyafahamu pia malengo ya Serikali ni yapi kwa sababu fursa zipo nyingi lakini zisipotangazwa hakuna atakayezifahamu,” amesema Mhandisi Samamba.

By Jamhuri