Na John Mapepele.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa maelekezo kumi yatasaidia kuimarisha sekta ya nyuki ili iweze kuchangia mapato ya Serikali na kwenye uchumi wa taifa kwa ujumla

Mhe. Mpango ametoa maelekezo haya leo Mei 20,2024 kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya nyuki duniani iliyofanyika jijini Dodoma ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda wamepewa tuzo maalum na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuthamini na kutambua mchango wao kwenye sekta.

Katika maelekezo yake ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana Wizara ya TAMISEMI kuyatambua maeneo maalum yenye fursa za kipekee katika eneo la mkoa wa Dodoma na Singida ili kuyahifadhi kisheria na kuwaelimisha wananchi wanaoishi katika maeneo hayo ambayo yana sifa ya uoto wa vichaka vya Itigi ambavyo duniani vinapatikana Tanzania na Zambia pekee.

Mhe. Mpango ameitaka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na Mfuko wa Misitu nchini(TAFF) kuwawezesha wananchi kwa kuwapatia mafunzo ya ufugaji nyuki na kuwapatia mizinga ya kisasa ili waweze kufuga kisasa.Pia ameelekeza Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania(TAFORI) kufanya tathinini mpya ya sekta ya Misitu na Nyuki ili kujana mipango ya kuendeleza sekta hizo.

Aidha, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kuja na mpango maalum wa ufugaji wa nyuki,kuendeleza program ya upandaji wa miti ambapo pia ameelekeza TAMISEMI kupitia Halmashauri zake zenye fursa ya ufugaji nyuki kote nchini kuajili wataalam watakao toa huduma ya ugani kwa wananchi na Wizara inayohusika na Kilimo kuandaa mkakati wa uchavushaji katika mazao.

Kuhusu Wizara ya Fedha , Mhe. Mpango ameitaka kuandalina namna ya kupunguza kodi kwenye vifaa katika mnyororo wa uchakataji wa asali, huku pia akiielekeza Wizara inayohusika na Mambo ya Nje kuzielekeza Balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kutafuta masoko ili kupata fedha za kigeni kupitia zao hili la asali.

Wakati huohuo amevitaka vyuo vya mafunzo ya nyuki nchini na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)kuwatumia wajasiliamali wanaofanya vizuri ili kuwafundisha wadau wengi zaidi. Ametoa rai kwa watanzania wote kuhamasika na kuanza kutumia mazao yatokanayo na nyuki ili kuboresha afya zao, pia wasanii na waandishi wa habari kuwatembelea.

Awali akimkaribisha Mhe. Mpango ilia some hotuba yake Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angelah Kairuki amesema Sekta hiyo kupitia nyuki imekuwa na mchango mkubwa katika eneo la uzalishaji wa mazao ya chakula. Matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika ndani ya Nchi zinaonesha kuwa kuwa zaidi asilimia 80 ya mimea ya chakula inayolimwa hapa nchini huchavushwa na nyuki

Aidha, amesema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa sekta ya nyuki pia inachangia takribani ajira 2,000,000 hasa kwenye eneo la ufugaji nyuki, usindikaji na biashara ya mazao ya nyuki katika soko la ndani na nje ya Nchi.

Amefafanua kuwa katika maadhimisho ya mwaka huu wizara yake imedhamiria kuhakikisha kuwa jamii inatambua mchango wa nyuki kwenye afya na maendeleo. ambapo, Kauli mbiu ya Kitaifa ya maadhimisho haya ni “Nyuki kwa Afya na Maendeleo, Tuwatunze.” (#APIMONDIA 2027 Tanzania Ipo Tayari)”.

Maadhimisho haya pia yamehudhuriwa na Mhe. Suleimani Jaffo Waziri wa Ofisi ya Makamu wa RAIS, Muungano na Mazingira, Mhe. Najma Giga, Makamu Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Wawakilishi wa wa Wakuu wa Mikoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Naibu wake CP. Benedict Wakulyamba, Wakuu wa Wilaya za Dodoma, Wakuu wa Taasisi,Viongozi wa dini na Viongozi wa vyama vya siasa, huku yakitanguliwa na maonesho maalum ya wadau wa sekta ya nyuki.