Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Watoto 45 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yakiwemo matundu kwenye moyo, na matatizo ya mishipa ya damu kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalum inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids lililopo nchini Marekani.
Kambi hiyo maalumu ya siku tano iliyoanza jana inatarajiwa kutoa matibabu ya upasuaji wa moyo wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab kwa watoto 25 na upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua kwa watoto 20.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Stella Mongela amesema upande wa cathlab watoto 25 watapatiwa matibabu ya kuziba matundu mbalimbali yaliyopo katika kuta za moyo pamoja na kufungua mishipa ya damu iliyobana inayopeleka damu kwenye mapafu na kwenye mwili.
Dkt. Stella amesema kupitia kambi mbalimbali zinazofanyika JKCI zimekuwa zikitoa fursa kwa madaktari wazawa kuendeleza ujuzi wao kwani wamekuwa wakikutana na mabingwa waliofanya kazi kwa muda mrefu hivyo kuongeza ujuzi zaidi.
“Kambi ya wataalamu wa afya kutoka Shirika la Mending Kids ni moja ya kambi inayotupa nafasa wataalamu wa JKCI kujifunza mbinu mbalimbali za kutoa huduma bora za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto”, amesema Dkt. Stella.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Felix Shonyela amesema Idara ya upasaji mkubwa wa moyo imepanga kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto kati ya watatu hadi wanne kila siku wakati wa kambi hiyo maalumu.
Dkt. Shonyela amesema wakati wa kambi maalumu watafanya upasuaji wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yakiwemo matundu katika moyo na mishipa ya damu ambayo haiko sawa inayopeleka damu kwenye mapafu.
“Katika kambi hii tutaenda kurekebisha mishipa ya damu ambayo haiko sawa inayoelekea kwenye mapafu na kupelekea mishipa mingine inayochukua damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye mapafu kuwa midogo, tunarekebisha mishipa hiyo ili damu iweze kwenda vizuri kwenye mapafu”, amesema Dkt. Shonyela.
Dkt. Shonyela amesema watoto ambao mishipa yao ya damu haiko sawa mara nyingi wakiwa wanafanya michezo huchoka kwasababu hakuna mbadilishano mzuri wa hewa ya oksijeni katika mapafu kwasababu damu inayokwenda katika mapafu inakuwa kidogo.
Naye mzazi ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi hiyo kutoka Mkoani Tanga Herieth Mbelwa alisema wazazi wengi wamekuwa wakiogopa kusikia watoto wao wanaumwa magonjwa makubwa kama ilivyo magonjwa ya moyo hivyo kuacha kuwapeleka Hospitali na kuwatibu kwa miti shamba.
Herieth amesema mtoto wake ana miaka minne na amekuwa akitibiwa shida ya nimomia hadi mwaka huu alipoamua kufika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na mtoto kugundulika kuwa na tundu kwenye moyo.
“Naamini kupitia kambi hii baada ya upasuaji ambao mtoto wangu kafanyiwa jana utaenda kuondoa changamoto alizokuwa akipitia kama za ukuaji, kutokuongezeka uzito, kuchoka na kushindwa kucheza”, amesema Herieth.
Kambi hiyo iliyoanza jana tayari imeshatoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto saba ambapo watoto watatu wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na watoto wanne wamefanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab.