Watu 111 wamekufa na wengine zaidi ya 230 wamejeruhiwa kufuatia tetemeko la ardhi lililopiga eneo la kaskazini magharibi mwa China la Gansu-Ginghai usiku wa kuamkia leo.

Kituo cha Ulaya cha kufuatilia mitikisiko ya ardhi duniani EMSC kimesema, tetemeko hilo la ardhi lilikuwa la ukubwa wa 6.1 katika kipimo cha Ritcha.

Kituo hicho kimeendelea kueleza kuwa, tetemeko hilo lilikuwa na kina cha kilomita 35 huku kitovu chake kikiwa kilomita 102 eneo la kusini magharibi mwa mji wa Lanzhou.

Shirika la habari la serikali Xinhua limeripoti kuwa, tume ya kitaifa ya China ya kukabiliana na majanga pamoja na wizara ya usimamizi wa dharura imeanzisha mpango wa mwitikio wa dharura wa kiwango cha nne kufuatia zilzala hiyo.

Tayari timu maalum imetumwa katika maeneo yalioathirika na tetemeko hilo la ardhi ili kutathmini athari zilizojitokeza na kutoa mwongozo wa zoezi la uokoaji na kupeleka misaada.