Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ametoa maagizo hayo leo Desemba 18, 2023 wakati wa mkutano maalum wa kimkakati na watumishi wa TRA katika Ukumbi wa Suma JKT, Mwenge-DSM.

RC  Chalamila amesema kodi ni chanzo cha mapato serikalini  hivyo aliwataka mameneja na maafisa wa TRA kwa ujumla wao kufanya kazi zao kwa weledi, kufuata sheria na kutoa elimu kwa umma ili kila mtu ajue umuhimu wa kulipa kodi kwa hiyari bila shuruti yoyote kwa masilahi mapana ya mtu mmoja mmoja naTaifa la Tanzania. 

“Kwa mfano wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka chuo kikuu leo katika mkoa wa DSM napokea si chini ya bilioni 1.2 kila mwezi kama ada na posho kwa walimu. Maana yake TRA tusipokusanaya kodi hii kwa mujibu wa sheria watoto hawa hawatapata huduma hizo,” amesema RC Chalamila.

Aidha RC Chalamila amewahimiza watumishi hao kufuatilia mashine EFD sababu kuna wafanyabiasha wengine huamua wao wazitumie au wasizitumie, “Hebu mahali popote ambapo hakuna matumizi ya namna hii tuendelee kuwa wakali.”

Mhe Chalamila alitoa rai kwa wafanyabiashara walipe kodi kwa hiyari kwa mujibu wa sheria zilizopo na wasisubirie nguvu ya polisi itumike, “Uwekezaji unaokwepa kodi haustahili kwenye nchi,” alisistiza.

Vilevile RC alisema kipindi kijacho ni kipindi cha chaguzi hivyo aliwaasa watumishi waendelee kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria bila kukatishwa tamaa na wanasiasa  kwakuwa kodi ndizo hutumika kufanya maendeleo na kupitia hayo maendeleo ndiyo kura kwa chama.

By Jamhuri