Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kisarawe

Mwanamke mmoja (35-40)pamoja na mtoto wa miezi sita wamefariki dunia iliyotokea Daru Mzumbwi Kisarawe ,baada ya basi lenye namba za usajili T 275 DRZ aina ya tata kutumbukia kwenye mto na kusababisha vifo hivyo.

Aidha watu wengine takribani hamsini wamejeruhiwa katika ajali hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani,Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Desemba 18, alasiri eneo la Daru Mzumbwi baada ya basi hilo, lililokuwa likitokea Kigogo freshi, kuelekea Mloka kupitia Kisarawe kupinduka na kuingia kwenye mto wenye maji.

“Basi lenye namba za usajili T 725 DRZ aina ya Tata likifanya safari zake Kigogo Dar es salaam- Mloka Rufiji ikiendeshwa na Juma Mohammed (51) mkazi wa Pugu Dar es salaam liliacha barabara na kutumbukia mtoni,”amefafanua Lutumo.

Lutumo ameeleza kwamba ,waliofariki dunia ni wawili akiwemo mwanamke mwenye umri unaokadiriwa miaka 35-40 na mtoto wa miezi sita.

Ametaja chanzo cha ajali hiyo ni dereva kushindwa kumudu gari kenye mteremko wenye kona kali.

Vilevile, Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge amefika hospitali ya Wilaya ya Kisarawe kuwapa pole na kuwajulia hali majeruhi waliokuwa katika ajali hiyo.

Akithibitisha kupokea majeruhi na miili ya marehemu ,Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya ya Kisarawe Dkt.Risasi Rajabu, ameeleza kuwa baadhi ya majeruhi waliopata majeraha madogo wamesha waruhusu na wengine wanaendelea kuwapatia matibabu.

Ameeleza, wengine saba wamewapatia rufaa ya kwenda hospitali ya rufaa Muhimbili.

Mkuu wa wilaya hiyo, Fatma Nyangasa ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa vituo vya dharura ambavyo leo hii kimeweza kuokoa maisha ya watu .

Kwa upande wake majeruhi ambae ni mama was kichanga kilichofariki Mwanahamisi Juma alieleza hakumbuki kilichotokea zaidi ya kujikuta akiwa kwenye maji mtoni.

“Nilikuwa na mwanangu wa miezi sita lakini sijui anaendeleaje na hali yake, hadi hapo nitakapojulishwa na daktari”ameeleza Mwanahamisi.

By Jamhuri