Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini Yahya Ahmed Okeish, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 19 Desemba 2023.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema uhusiano baina ya Tanzania na Saudi Arabia umeendelea kuimarika na mataifa hayo kuendelea kushirikiana katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa. Makamu wa Rais amesema Tanzania inatambua mchango unaotolewa na nchi ya Saudi Arabia katika ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Saudi pamoja na kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu.

Makamu wa Rais amesema ni muhimu mataifa hayo mawili kuongeza ushirikiano katika masuala ya biashara na uwekezaji. Amemsihi balozi huyo katika kipindi atakachohudumu nchini Tanzania kuwezesha ongezeko la makampuni mbalimbali ya Saudi Arabia kuwekeza nchini Tanzania pamoja na kuongeza idadi ya watalii kutoka taifa hilo.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Tanzania na Saudia Arabia zinaweza kushirikiana katika sekta ya mafuta na gesi kwa kuzingatia uzoefu wa taifa la Saudi Arabia katika sekta hiyo. Pia ameikaribisha Saudi Arabia kushirikiana na Tanzania katika sekta ya madini hususani madini ya kimkakati yanayoweza kusaidia katika kupatikana kwa nishati safi na hivyo kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Pia amesema ushirikiano unahitajika katika kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu ili kuweza kutumia vema rasilimali nyingi zilizopo Tanzania.

Makamu wa Rais ameipongeza nchi Saudi Arabia kupitia Balozi huyo kwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya mwaka 2030 (Expo 2030). Aidha amesema Tanzania imefurahishwa na uwepo wa usafiri wa ndege wa moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Tanzania ambao unaimarisha mahusiano yaliyopo baina ya mataifa hayo mawili.

Kwa upande wake Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini Mheshimiwa Yahya Ahmed Okeish amesema Tanzania na Saudi Arabia zimekua na mahusiano ya kihistoria na kibinadamu ambayo yameendelea kuimarika. Ameongeza kwamba Saudi Arabia inachukulia kwa umuhimu wa kipekee mahusiano yake na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.

Amesema kutangazwa kwa nafasi 500 za ajira za wauguzi Watanzania nchini Saudia Arabia ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliyopo na ziara aliyoifanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini humo. Ameongeza kwamba katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Saudi Arabia imeweka mpango wa kushirikiana katika kupatikana kwa nishati safi ya kupikia hivyo itashirikiana na Tanzania kwa kuzingatia mpango huo umeanzishwa pia na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Balozi Okeish amesema atafanya kazi kwa kushirikiana vema na Tanzania kuhakikisha watalii kutoka nchini Saudia Arabia wanaongezeka. Pia amesema Saudia Arabia inatambua nguvu kazi iliyopo Afrika ikiwemo Tanzania na lengo ni kushirikiana katika kutumia vema nguvu kazi hiyo.