Watu 15 wa familia moja wamefariki nchini Namibia baada ya kunywa uji ambao maafisa wanaamini ulikuwa na sumu.

Hili ni miongoni mwa matukio mabaya zaidi nchini humo ya maafa yanayotokana na chakula kibovu.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa familia hiyo ambayo ilikuwa imepigwa na njaa kupitiliza ilikunywa uji huo kutoka kwa mabaki ya nafaka ya kutengeneza pombe.

Polisi wanasema kuwa wanatoka katika familia ya watu 21 katika kijiji kimoja eneo la Kavango Mashariki linalopatikana Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa msemaji wa Polisi kuna Shikwambi,watu hao 15 waliofariki walianza kuugua baada ya kula mnamo Jumamosi na kukimbizwa hospitalini.

“Kufikia sasa hii ndio idadi kubwa zaidi ya vifo kuwa kutokea kwa sababu ya kula chakula chenye sumu au kilichoharibika,” Shikwambi amenukuliwa na AFP.

Shirika la Utangazaji la Nambia, NBC limeripoti kuwa uji huo ulichanganywa na kitu kilichochacha kilichobaki kutoka kwenye kinywaji cha pombe kilichotengenezwa nyumbani.

Kwa mujibu wa NBC, watu wengine wanne wako katika hali mbaya na wamelazwa hospitali. Likiinukuu wizara ya afya, shirika hilo la utangazaji limesema takribani watu 20 walikunywa uji huo wenye sumu baada ya kuchanganywa na mabaki ya bia ya kutengenezwa nyumbani.

Wahanga wana kati ya umri wa miaka miwili hadi 33. Tukio hilo limetokea katika jimbo la Kavango Mashariki, kaskazini mashariki mwa Namibia.