Wanaume wawili waliokuwa na matatizo ya  nguvu za kiume kutokana na matatizo mbali mbali ya kiafya, wamefanyiwa upasuaji na kupandikizwa uume katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkoji nchini (TAUS) pamoja na Daktari bingwa kutoka nchini Ufaransa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa leo Juni 14, 2023  inasema kuwa upasuaji huo wa kupandikiza uume umefanyika katika hospitali hiyo iliyopo mkoani Dodoma kwa mara ya kwanza.

Akizungumza mara baada ya upasuaji huo, Daktari Bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa Remigius Rugakingira amesema upandikizaji huo wa uume umefanyika kwa mara ya kwanza nchini.

“Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufanya upasuaji wa aina hii kilichofanyika hapa ni kuweka vipandikizi maalumu vitakavyowezesha uume kurudi katika hali yake ya kufanya kazi.” amesema

Dkt. Rugakingira amesema Hospitali ya Benjamin Mkapa inajali afya ya Wanaume na upasuaji kama huu unaweza kufanyika Tanzania na kuwataka wanaume wenye matatizo ya nguvu za kiume kufika hospitali ya BMH kufanya upasuaji wa kuweka vipandikizi kwenye uume kwani ndio hospitali pekee kwa sasa inayotoa huduma hiyo hapa nchini.

Kwa upande wake Dkt. Liuba Nyamsogolo ambae ni kiongozi wa chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo (TAUS) amesema kuwa wamefikia hatua hii kutokana na uwepo wa watu wengi wenye matatizo ya nguvu za kiume nchini na Afrika kwa ujumla.

“Moja wapo ya dhumuni ya TAUS ni kuendeleza wataalam nchini kwa kushirikiana ma wataalam kutoka nje ili kuleta teknolojia inayopatikana duniani nchini Tanzania na kutibu magonjwa kama haya kwa wale wenye matatizo,” alisema Dkt. Nyamsogolo.

Msemaji wa BMH eremiah Mbwambo amesema “Hospitali ya BMH imekua Hospitali ya kwanza nchini kufanya upasuaji wa kuweka vipandikizi kwenye uume kwa wagonjwa wenye matatizo ya nguvu za kiume, serikali ya awamu ya sita imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuiwezesha teknolojia za kisasa za matibabu ili kuwapatia matibabu thabiti wananchi”

By Jamhuri