Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Sal

Wazazi , viongozi wa dini na wale wa kimila pamoja na wadau mbalimbali nchini wametakiwa ,kusimamia malezi ya vijana na watoto wa wa kike na kiume ili waweze kuwa na maadili bora .

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa kituo cha Usuluhishi (CRC) Gladness Munuo,wakati alipokuwa akizungumza na Jamhuri mara baada ya mkutano ulioandaliwa na kituo hicho kwenye ukumbi wa Hekima Garden- Dar es Salaam leo ulio washirikisha wadau mbalimbali kujadili masuala ya uzazi salama kwa vijana kundi rika.

Gladness amesema maisha ya sasa kwenye malezi na ukuaji wa teknolojia yamekuwa tofauti na miaka ya nyuma, kwa sababu kuna sehemu ambayo malezi makuzi hayajakaa sawa kwenye jamii kutokana na wazazi kuwa na muda mwingi wa utafutaji wa maisha ( pesa). “Wengi tunasahau majukumu yetu na kuwapatia si makuzi tu hata malezi bora, Ili watoto wetu wawe mama bora na baba bora wa baadaye.”

Gladness amesema kwa sasa changamoto ya mitandao ya kijamii, TV na simu imekuwa mwiba kwa watoto kuharibika kimaadili, kwa sababu huko kuna mafunzo mazuri na mabaya kwa hiyo utakuta wanapata mafunzo ambayo sio sahihi kwa maisha yao ya baadae.

“Kama wazazi tunatakiwa kuangalia vijana wetu wanaishi vizuri ,wanakuwa na vizazi vilivyo salama na vyenye maadaili. Leo tumezungumzia masuala ya ndoa za utotoni, mimba za utotoni na zisizo tarajiwa ambazo Kwa sasa zimekuwa tatizo kubwa sana pengine tuna haja sasa kuchukua hatua za kuhakikisha tunarejesha hali kuwa salama.”

Tumewashirikisha wadau hasa viongozi wa dini na kimila Kwa kuwa wao nyuma Yao wana jamii inayowasilikiza kwa wingi, tunaamini watatusadia kupeleka ujumbe huo kwa wazazi na jamii kwa ujumla.

Alphonce Isakwi kutoka kituo cha kisheria msaada wa kisheria Kinondoni- (Kinondoni ‘Paralegal’) amesema kwa sasa kiumbe Mwanaume yuko hatarini kutoweka kutokana na watoto wa kiume kukabiliwa na changamoto kubwa ya kunyanyaswa kijinsia lakini pia kugubikwa na uvivu na kuishia kubadilisha jinsi kinyume na maadili ya Dini lakini pia Mila na Desturi zetu.

“Unajua zamani watoto waliokuwa wanafanyiwa ukatili mkubwa ni wa kike, lakini sasa hivi wanaofanyiwa sana idadi kubwa ni watoto na vijana ni wa kiume. Kutokana na vitendo hivyo wapo walevwanaodhamiria kabisa kuua kizazi, Kwa maana baadaye wanakuwa hawafai kuwa wanaume kamili na Baba Bora na wengi baada ya vitendo wanajikuta anaingia kwenye ushoga”, amesema.

Mwezeshaji wa majadiliano hayo Idda Swai amesema Vijana wa kike wanakabiliana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kujamiiana kusiko salama, hii huwapelekea kupata mimba za mapema magonjwa ya ngono (STI), VVU/ UKIMWI na utoaji wa mimba usio salama.

Amesema kwa sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi kumi za kusini mwa Bara la Afrika yenye changamoto kubwa katika afya ya uzazi kwa vijana.

“Tafiti zinaonyesha kufikia umri wa miaka 19 wasichana waliowengi hupata mimba au kujifungua na VVU/UKIMWI/STI unaongezeka miongoni mwa vijana wenye umri mdogo ukilinganishwa na wanaume ambapo watoto au mabinti huathirika mara mbili kuliko wanaume.”

Tanzania inakadiriwa kuwa na vijana balehe kuanzia umri wa miaka 10 mpaka 19 wapatao milioni 14 ( Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022/Tanzania 2022, Tanzania population and Housing Sensa)

Asilimia 77 ya watanzania ni vijana wa umri wa chini ya miaka 35 na asilimia 34.7 ni vijana kati ya miaka 15 na 35.( Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022/Tanzania 2022, Tanzania population and Housing Sensa)

Mikoa inayoongoza kuwa na vijana wengi wenye umri wa miaka kati ya 15 na 35 kutokana na makadirio ya sense ya watu na makazi ya mwaka 2022 ni Tanga, Iringa, Njombe, na Rukwa. Ikifuatiwa na Ruvuma, Singida, Shinyanga, Kilimanjaro, Arusha, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, na Mjini Magharibi.

Umri wa balehe ni muda mzuri wakujenga tabia za kujali afya na mitindo. ya maisha inayohusiana na Afya ya Uzazi, kwa kuwa ni kipindi cha mabadiliko ya kimwili, kihisia na kijamii, pia ni kipindi ambacho vijana hugundua ujinsi wao na kujenga mahusiano na wengine.

Ili kudumisha afya ya uzazi vijana wanahitajika kupata taarifa sahihi kuhusu njia salama na bora, na nafuu na zinazokubalika za kupanga ni lini atahitaji mtoto, ni nani wa kupata nae mtoto, na idadi ya watoto wanaowahitaji. (Uzazi wa mpango/Family planning)”amesema

Amesema ni muhimu vijana wapewe taarifa za kuwawezesha kujikinga na magonjwa ya zinaa. Kila mtu ana haki ya kufanya uchunguzi wake mwenyewe kuhusu afya yake na tendo zima la kujamiiana na uzazi salama