Na WMJJWM, Dar es Salaam

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa pili wa kutokomeza Ukeketaji ambao unatarajia kuwa na washiriki 900 kutoka Barani Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 07, 2023 jijini Dar es Salaam, Waziri Dkt. Gwajima amesema, Tanzania imechaguliwa kuwa nchi mwenyeji wa Mkutano huo utakaofanyika kuanzia Oktoba, 09 hadi 11, 2023 kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere.

“Kwa mwaka huu wa 2023, Tanzania tumepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa kutokomeza ukeketaji ambapo kama nchi tutakuwa na washiriki 200 kutoka mikoa yetu yote na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Afrika na Mabara mengine watakuja washiriki 700” amesema Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima amefafanua kuwa Mkutano huo utakaokuwa na Kaulimbiu isemayo “Mabadiliko katika kizazi kimoja kwenda kingine ni muhimu katika kutokomeza vitendo vya ukeketaji” (Changes in a Generation) una lengo la kutoa fursa kwa wadau wanaopambana na ukeketaji kuunganisha nguvu za pamoja, kubadilishana uzoefu, kujengeana uelewa na maarifa katika kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukeketaji katika nchi za Afrika.

Kwa mujibu wa Dkt. Gwajima amesema, wakati wa mkutano huo kutafanyika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, ambayo ufanyika Oktoba ya kila mwaka.

Maadhimisho hayo ni ya 12 tangu kuanza kuadhimishwa ni utekelezaji wa Tamko la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Na. 66/170 la tarehe 19 Desemba, 2012. Lengo la siku hiyo ni kutathmini jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kuboresha upatikanaji wa Haki, Ulinzi, Ustawi na Maendeleo ya Mtoto wa Kike.

Akifafanua kuhusiana na hali ya kitakwimu kwenye masuala ya Ukeketaji nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Sebastian Kitiku amesema kwa sasa ni takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa Manyara una asilimia 58, Dodoma asilimia 47, Arusha asilimia 41, Mara asilimia 32, Singida asilimia 31 na Tanga Asilimia 14 hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanashirikiana katika kutoa elimu kwa jamii ili vitendo hivyo vitokomee nchini.

Tanzania ilipata fursa ya kushiriki Mkutano wa kwanza wa Kimataifa wa Kutokomeza Ukeketaji nchini Burkina Faso mwaka 2018 ambao ulishirikisha jumla ya nchi 22 wanachama wa Umoja wa Afrika.

Mkutano huo uliazimia kwamba kila kanda katika Afrika ianzishe ushirikiano wa kupambana na mila na desturi ya ukeketaji sambamba na kudhibiti mipaka kuzuia mwingiliano wa mila hiyo kutoka nchi moja kwenda nyingine (Crossboader FGM) na mkutano kama ule unafanyika kila baada ya kipindi fulani katika nchi inayoteuliwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika.