Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe

Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, imewahukumu kunyongwa hadi kufa washtakiwa tisa akiwemo Beatus Salum aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Kipengere Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe kwa makosa ya mauaji ya ndugu wawili mwaka 2020 kijijini hapo.

Hukumu hiyo ya kesi ya mauaji namba 11 ya mwaka 2019 imetolewa na hakimu Zabibu Mpangule mbele ya washtakiwa,mawakili wa utetezi na mwendesha mashtaka ambapo amesema kwa kuzingatia makosa ya mauaji ya watu wawili Francis Chaula na Fabio Chaula ambao ni mtu na kaka yake mahakama hiyo imewahukumu washtakiwa wote kunyongwa hadi kufa.

“Kwa kuzingatia kwamba hapa kuna makosa mawili ya mauaji ya watu wawili wasiokuwa na hatia mahakama hii kwa kila kosa inawahukumu washtakiwa wote kunyongwa hadi kufa sawa sawa na kifungu namba 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 ya 2022 hata hivyo kama kuna upande una haja ya kukata rufaa hiyo ndani ya muda”amesema Hakimu Mpangule.

Amesema kifupi mnamo Aprili 27, 2020 katika Kijiji cha Kipengere ndani ya Wilaya ya Wanging’ombe washtakiwa wote waliwaua Francis Frank Chaula na Fabio Frank Chaula ambapo taarifa za uchunguzi wa miili hiyo iliyotolewa na daktari ni kuwa sababu vifo vimetokana na kuvuja damu nyingi uliosababishwa kupigwa na vitu vizito.

Hakimu amesema mshtakiwa namba 6,7,8 na 9 ambao walikuwa ni viongozi akiwemo mwenyekiti wa kijiji,mtendaji wa kijiji pamoja na mwenyekiti wa CCM tawi wao wanaingia katika hukumu hiyo kutokana na kufanya vikao vilivyokuwa vikihusu mauaji kama ilivyoelezwa na mshtakiwa namba 5 kwenye kesi hiyo wakiwa na kisasi cha kumuua Frank Chaula ambaye ni baba wa watoto hao kwa sababu amekuwa akiwasumbua katika maeneo tofauti tofauti.

Awali hakimu Mpangule akitaja majina ya washtakiwa amesema miongoni mwa washtakiwa hao ni pamoja na Fabian Chaula,Geoffrey Ilomo,Aurelius Mgaya, Richard Chaula,John Bosco, Otumary Mtivike na Beatus Salum.

By Jamhuri