Sisi wananchi wa Nyasirori, Butiama mkoani
Mara, tunaomba kujua faida za huu mgodi
wa dhahabu kijijini kwetu.
Tangu kuanzishwa kwa mgodi huu kwa
kweli hatuoni mafanikio yoyote ya maana
kwetu wananchi wa kawaida.
Tunachokiona ni baadhi ya viongozi wa
kitaifa kuingia na kutoka mgodini bila
kueleza wananchi mafanikio gani
tutakayopata kutokana na uwekezaji huu.
Hapa ikumbukwe kuwa ujio wa hawa
wawekezaji umetuumiza baadhi yetu
wananchi kwa kutoa ardhi ambayo ilikuwa
inatufaa kwa shughuli mbalimbali za
kiuchumi.
Pamoja na kuwa na mgodi huu, hali za
wananchi bado ni mbaya. Hatuna huduma
za matibabu za kueleweka wala shule za
msingi zenye vifaa vya kisasa.
Wengine katika mikoa ya Simiyu,

Shinyanga, Mwanza, Geita na Tabora
tunasikia wawekezaji wakifanya mambo
mbalimbali ya kimaendeleo kwa ajili ya
wananchi. Je, sisi wananchi wa Nyasirori si
Watanzania?
Jambo jingine linalotupa shaka ni uhusiano
wa viongozi wa mgodi na wa serikali. Shaka
yetu inazidi kwa sababu wakati magari ya
mgodi huu yalikamatwa yakisafirisha
dhahabu, lakini yaliachiwa katika mazingira
yasiyoeleweka vizuri.
Wananchi hatukuambiwa magari hayo
ambayo yalikamatwa Kiabakari yalikuwa
yamebeba mali kiasi gani, na hatima ya mali
hiyo pamoja na wawekezaji hawa
waliotuhumiwa ni nini. Je, tuamini kuwa
viongozi wetu walipewa chochote na
kuamua kuzima mambo hayo mabaya?
Waziri wa Madini, Angela Kairuki na naibu
mawaziri tunaomba waje Nyasirori.
Wasiishie Mirerani tu kwenye tanzanite,
maana kila uchao utasikia wako huko au
wako Epanko, Morogoro.
Kama hawatakuja tutajua lao ni moja na
wawekezaji ambao si wakweli kwenye suala
la kuhakikisha rasilimali za nchi
zinawanufaisha wananchi wazawa.
Tunaomba Waziri Kairuki aje mapema,

kwani tunasikia kuna mipango mingine ya
kupanua migodi ya dhahabu huku katika
eneo la kata na wilaya yetu.
Mwisho, naomba jina langu lihifadhiwe kwa
sababu wakinijua nimeandika taarifa hii
naweza kufia gerezani.

Mimi mkazi wa Nyasirori,
Butiama, Mara.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share