Na James Mwanamyoto,JamhuriMedia,Dodoma

Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Ridhiwani Kikwete ameitaka Idara ya Mishahara,Motisha na Marupurupu kubuni njia mbalimbali za kutoa motisha kwa watumishi wa umma ambazo zitatumiwa na waajiri Serikalini ili kuwajengea ari na morali ya kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Kikwete ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa idara hiyo kilicholenga kufahamu majukumu yanayotekelezwa na kuhimiza uwajibikaji.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akizungumza na watumishi wa Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa Idara hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kufahamu majukumu ya Idara hiyo na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Idara hiyo.

Kikwete amesema, zitafutwe njia nzuri na sahihi za kuwapa motisha watumishi wa umma ambazo hazitaathiri bajeti ya utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali pamoja na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa lengo la kuboresha miundombinu ya utoaji huduma muhimu kwa wananchi.

Kikwete amefafanua kuwa, motisha kwa watumishi wa umma si lazima iwe fedha bali inaweza kufanyika kwa kuboresha mazingira ya kazi kwa kuwapatia watumishi wa umma vitu mbalimbali kwa mfano bima ya afya ya uhakika itakayowawezesha kupata huduma bora ya matibabu na kuimarisha afya ili waendelee kuwahudumia wananchi ipasavyo.

“Motisha isijikite sana kwenye fedha, izingatie pia kuboresha mazingira ambayo yatamuwezesha mtumishi wa umma kutekeleza majukumu yake kikamilifu,” amesisitiza.

Mkurugenzi wa Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu, Mariam Mwanilwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Idara yake kwa Naibu waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa Idara hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kufahamu majukumu ya Idara hiyo na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Idara hiyo.

Kikwete ameongeza kuwa, yeye binafsi anaamini kwamba licha ya mtumishi wa umma kupata stahiki ya mshahara wake lakini motisha kwa mtumishi wa umma ni jambo muhimu sana katika kumuongezea ari, morali na ufanisi wa utendaji kazi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuujenga utumishi wa umma unaowajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma bora, hivyo motisha kwa watumishi wa umma ni sehemu ya kulifikia lengo la kuujenga utumishi wa umma unaowajibika kwa umma.

Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Mishahara na Motisha, Bwana Ghubas Vyagusa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya sehemu yake kwa Naibu waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kufahamu majukumu ya Idara hiyo na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Idara hiyo.

By Jamhuri