Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limetangaza nafasi za kujiunga na Jeshi hilo kwa vijana Watanzania wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne hadi Shahada ya Uzamili ambao wamemaliza Mkataba wa Mafunzo ya kujitolea katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kurudishwa majumbani.

Akitoa taarifa hiyo mbele ya Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO leo jijini Dodoma (Machi 9, 2023), Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda amebainisha sifa za mwenye nia ya kuandikishwa anatakiwa kuwa raia wa Tanzania wa kuzaliwa mwenye kitambulisho cha Taifa, awe na umri wa miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha nne hadi cha sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu pia awe na afya nzuri na akili timamu.

Luteni Kanali Ilonda ameongeza “Awe Mtanzania mwenye tabia na nidhamu nzuri, hajapatikana na hatia ya makosa ya jinai mahakamani na kufungwa, awe na cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti vya shule na taaluma, awe hajatumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo, awe amehitimu Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mkataba wa Kujitolea miaka miwili na kutumikiwa cheti na asiwe ameoa au kuolewa”

Aidha, Kaimu Mkurugenzi huyo wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Ilonda amesisitiza “Maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe Makao Makuu ya Jeshi, Dodoma kuanzia tarehe ya tangazo hili yaani leo tarehe 09 Machi, 2023 hadi tarehe 20 Machi, 2023 yakiambatishwa na nakala ya kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA, nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na chuo, nakala ya cheti cha JKT na namba ya simu ya mkononi ya mwombaji”.

Sambamba na hilo, maombi yatumwe kwa anuani ya Mkuu wa Utumishi, Makao Makuu ya Jeshi, sanduku la posta 194, Dodoma, Tanzania na baruapepe [email protected]