Na Hassan Mabuye,JamhuriMedia,Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amesherekea siku kuu ya Krisimasi na wagonjwa kwa kula nao chakula pamoja na kukabidhi zawadi za Krisimasi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Waziri Mabula amekabidhi zawadi hizo leo kwa wagonjwa katika wodi ya watoto walio na changamoto ya lishe na watoto walio na changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo watoto waliopata ajali za moto na majanga mbalimbali.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula akila chakula pamoja na wagonjwa na wauguzi wa wodi ya watoto wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, katikati waliokaa ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest.

“Nimeamua kuja kusherehekea sikukuu na wagonjwa kwa kuleta chakula nilichopika nyumbani kwangu, vinywaji na matunda kwa sababu najua leo ni siku kuu ya Krisimasi na ushiriki watoto ni muhimu lakini kuna ambao wameshindwa kusherehekea wakiwa nyumbani kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya” Amesema Dkt. Mabula.

Aidha, Waziri Mabula Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameonesha njia kwa viongozi kusherehekea siku kuu pamoja na wananchi wenye uhitaji ambapo ametoa huduma ya vyakula kwa mikoa yote nchini kwa ajili ya Krismasi na Mwaka Mpya ili watu wote waweze kupika na kusherehekea hata kama hawana uwezo kiuchumi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula (kushoto) akiongea na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest (kulia) pamoja na Bw. Stanley Mahumbo Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo (katikati).

“Na mimi namshukuru sana Mhe. Rais kwa sababu ameonesha njia toka jana mikoa yote amegawa vyakula kwenye vituo vya kulelea watoto kwa ajili ya sikukuu hizi za Krisimasi na Mwaka Mpya, na sisi kama wawakilishi wake ni wajibu wetu kuwatembelea wahitaji hasa watoto ndio maana nimeamua kuja hapa Hospitali kula nao sikukuu” Aliongeza Dkt. Mabula.

Katika ziara hiyo Waziri Mabula aliongozana na Dkt. Ibenzi Ernest Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma ambaye amemshukuru Waziri Mabula kwa sadaka yake hiyo ambayo amesema ni moja katika mchango mkubwa wa mgonjwa kufarijika pale ambapo anaona watu wanamjali.

Dkt. Ibenzi ametumia fursa hiyo kuumuomba Waziri Mabula kufikisha shukrani zake kwa Mhe. Rais kwa mafanikio makubwa ya kuboresha huduma za Afya hasa katika upatikanaji wa vifaa tiba na maboresho ya majengo ya utowaji huduma za afya katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula (katikati) akiongozana na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest (kushoto) wakati wakiwasili katika Hospitali hiyo.

“Kwa kweli sisi watoa huduma za afya tunaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa maboresho mengi yaliyofanyika kuanzia ukarabati Majengo, upatikanaji wa vifaa tiba vyakutosha na hata usafi katika wodi zetu, kwani zamani ilikuwa hospitali zina toa harufu kwa kutofanyiwa usafi kwa muda mrefu kwa sababu ya kukosa huduma za vifaa na dawa za kutosha” aliongeza Dkt. Ibenz.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akikabidhi zawadi za Krisimasi kwa mmoja wa mzazi wa mtoto aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma

By Jamhuri