Kuelekea msimu wa sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limepiga marufuku kuwepo kwa Disko toto huku likiagiza kufungwa kwa baa zote baada ya saa sita usiku, isipokuwa zile zenye vibali maalum.

Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama wakati wa sherehe za krismasi na Mwaka mpya Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi amewataka wazazi na walezi kuwajibikia jukumu la kuwasimamia vyema watoto katika kipindi hicho cha sikukuu.

Kamanda Magomi amesema baada ya saa sita usiku baa zote zitafungwa isipokuwa zitakazoendelea kutoa huduma ni zile zenye vibali maalum.

“Disko toto zimepiga marufuku na tutakwenda kwenye kumbi zote kuhakikisha kuwa hakuna disko toto na niwatake wazazi kuendelea kuwasimamia hawa watoto tusherehekee hizi sikukuu kwa amani na utulivu majumbani kwetu lakini siyo kuwapeleka kwenye disko toto watoto wetu”amesema ACP Magomi.

“Niwatake wazazi tusimamie watoto wetu sambamba na hilo sisi jeshi la polisi tumejipanga vizuri kusimamia sheria kwa maana ya kusimamia doria, misako na oparesheni mbalimbali kwahiyo walevi sheria iko wazi mwisho wa kunywa pombe unajulikana baada ya saa sita Bar zote zifungwe labda kwa zile ambazo zinavibali ndiyo wanaweza kuendelea sisi tutaendelea kusimalia hayo na wale wote ambao tutawabaini tutakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria” amesema ACP Magomi

Kamanda Magomi amesema jeshi hilo limejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga wanasherekea sikukuu za Krismas na Mwaka mpya kwa amani na utulivu ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye nyumba za ibada.

“Jeshi la Polisi tumejipanga vizuri kwenye ibada tutakuwepo kwa maana ya kuhakikisha ulinzi wa kila raia upo vizuri lakini pia tumejipanga vizuri kwa maana ya barabarani kwenye mitaa na sehemu zote za starehe kuhakikisha kuwa hizi sikukuu zinapita kwa hali ya usalama kabisa”amesema.