Na Munir Shemweta, WANMM Kwimba

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wanawake nchini kujiamini wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Dkt.Mabula amesema hayo tarehe 8 Machi 2023 wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Kwadeko wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (katikati) na Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima wakipokea maandamano wakati wa Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Kwadeko wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza tarehe 8 Machi 2023.

Amesema,wanawake wanatakiwa kufanya kazi zao huku wakielewa kuwa juu yao yupo mwanamke shujaa ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan aliyemueleza kuwa ameonesha kuwa wanawake wanaweza.

“Tulioko katika nafasi tunatakiwa kuangalia watangulizi wetu walichofanya kama vile akina Mongela na Asha-Rose Migiro na kila mwanamke anayepewa nafasi ya uongozi mahali fulani, anatakiwa kujiamini kwa kuwa wanawake wamemuweka pale” alisema Dkt Mabula.

Akigeukia upande wa sekta ya Ardhi Dkt.Mabula ameelezea azma ya rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kama mwanamke kuonesha kuwajali wananchi hasa pale alipoamua kutoa msamaha wa riba kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi ambapo msamaha huo ulianza julai hadi desema mwaka 2022 na baada ya muda huo kuisha aliongeza hadi April 30, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, uamuzi huo wa Rais Dkt.Samia unalenga kuwapa nafuu watanzania bila kujali jinsia zao ambapo alitoa wito kwa wadaiwa wote kutumia fursa iliyotolewa kulipa madeni na kusema muda huo ukipita hakuna haja ya kumlaumu rais wala wizara ya ardhi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Wa pili kulia), Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima (kulia) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mery Masanja (Kushoto) wakipokea maandamano wakati wa Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Kwadeko wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza tarehe 8 Machi 2023.

Naye mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo ya siku ya wanawake Duniani kimkoa alikemea masuala ya ukatili kwa watoto pamoja na jinsia na kusisitiza kuwa, akina mama wana wajibu wa kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kufuatilia hali za watoto wao kwa lengo la kutengeneza kizazi chenye usalama.

“Kuwepo utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii katika masuala ya yanoathiri akina mama katika jamii na kuanzia ngazi za chini ili kuitengenezea jamii uelewa’’ amesema Malima.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani katika mkoa wa Mwanza yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali na yaliambatana na michezo sambamba na kutoa misaada kwa akina mama wakiwemo wajawazito.

Watumishi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakipita mbele ya mgeni rasmi wakati wa Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika viwanja vya Kwadeko wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza tarehe 8 Machi 2023.

By Jamhuri