Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuepuka matumizi ya Dawa za Kulevya kwani yanaharibu nguvukazi ya Taifa hasa vijana ambao wanategemewa kuongoza kufanya shughuli za uzailishaji na kuharakisha maendeleo

Ametoa wito huo leo (Jumanne Aprili 2, 2024) katika sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika kitaifa Katika Viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi Mkoani Kilimanjaro.

“Idadi kubwa ya waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ni watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24. Kundi hili ni nguvukazi ya Taifa letu, Serikali, haiwezi kunyamaza itaendelea kufanya msako mkali ili wahusika wote wa biashara hiyo haramu wachukuliwa hatua kali”

Amesema kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu wa udhibiti wa biashara ya dawa ya kulevya imeendelea kuongeza kasi ya mapambano ili kukomesha biashara, kilimo na matumizi ya dawa za kulevya. “Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote wanaojihusisha na kilimo hicho haramu pamoja na biashara ya dawa za kulevya”

“Viashiria vya kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya nchini ni pamoja na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watumiaji wanaotafuta matibabu, kuongezeka kwa watu wanaokamatwa wakitumia dawa za kulevya, kiasi cha dawa za kulevya zinazokamatwa zikiingizwa nchini na kuwepo kwa uhalifu unaohusishwa na matumizi ya dawa za kulevya hasa uporaji, wizi na ukabaji.”

Amesema mbio za mwenge wa uhuru za mwaka 2024 zitaendelea kutoa hamasa kwa jamii kusitisha kilimo haramu cha bangi, biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Aidha, utajiekeleza kwenye kuhamasisha jamii kulima kilimo cha mazao halali ya biashara na chakula, pamoja na kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli nyingine halali na zenye staha.

“Hivi karibuni, kumeibuka aina nyingine ya bangi yenye kiasi kikubwa cha kilevi ikifahamika kama “skanka”. Aina hii ya bangi yenye sumu nyingi huchanganywa kwenye sigara na vijana wamekuwa wakitumia skanka ambayo imekuwa ikipelekea kuchanganyikiwa.”

Amesema kuwa vijana wamekuwa wakitumia bidhaa hizo wakifahamu uwepo wa skanka na wengine bila kufahamu na hujikuta wanakuwa waraibu wa bangi. 

Amesema Idadi kubwa ya waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ni watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24. 

“Kundi hili ni nguvukazi ya Taifa letu ambayo inategemewa kuongoza kufanya shughuli za uzailishaji na kuharakisha maendeleo ya Taifa.”

Amesema Serikali, itaendelea kufanya msako mkali ili wahusika wote wa biashara hiyo haramu wachukuliwe hatua kali, na kuongeza kasi ya mapambano ili kukomesha biashara, kilimo na matumizi ya dawa za kulevya.

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu utaendelea  kuhimiza mapambano dhidi ya Rushwa, huku akitoa wito kwa Watanzania kupambana na vitendo vya rushwa.

“Tafiti za taasisi za kitaifa na kimataifa zinaonesha kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa. Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti wa REPOA iliyotolewa Machi 9, 2022 Tanzania inafanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa ambapo zaidi ya asilima 77 ya Watanzania waliohojiwa walikiri kuwa rushwa imepungua nchini.”

Kadhalika, amesema Serikali kupitia mbio za mwenge itaendelea kuwashurikisha wananchi na wadau wengine  katika mapambano dhidi ya maambukizi ya mapya ya virusi vya UKIMWI.

“Watanzania wenzangu ninaomba mfahamu kuwa, afya zetu ndio mtaji wetu. Hatuwezi kufikia ndoto zetu tulizojiwekea kimaisha bila kuwa na afya njema, hivyo wananchi wote tushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya UKIMWI.”

Naye, Waziri wa Habari, Vijana Utanaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Tabia Mwita Maulid, Amesema mbio za mwenge wa Uhuru zimeendelea kudumisha Uhuru, amani mshikamano uzalendo na umoja wa kitaifa pia zimekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii.

Awali, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana ajira na wenye Ulemavu, Mheshimiwa Patrobas Katambi amesema falsafa ya Mwenge wa Uhuru imekuwa ni kuwaunganisha watanzania, kuleta matumaini pamoja na kukagua miradi inayotoa huduma kwa wananchi ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Please follow and like us:
Pin Share